• HABARI MPYA

    Friday, December 28, 2018

    SIMBA YAPANGWA NA AL AHLY, VITA NA TIMU YA ULIMWENGU LIGI YA MABINGWA

    Na Mwandishi Wetu, CAIRO
    KLABU ya Simba ya Tanzania imepangwa Kundi D pamoja na JS Saoura ya Algeria, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Katika droo iliyopangwa usiku huu ukumbi wa Nile Ritz-Carlton mjini Cairo nchini Misri, Kundi A limezikutanisha timu za na Lobi Stars ya Nigeria, Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
    Kundi B linaungwa na FC Platinums ya Zimbabwe, Horoya A.C ya Guinea, Esperance ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakati Kundi C limezikutanisha Ismailia FC ya Misri, CS Constantine ya Algeria, Club Africain ya Tunisia na TP Mazembe ya DRC.
    Mechi za hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa zitaanza Januari 11 mwakani na kufikia tamati Machi 17. Droo ya Robo Fainali itafanyika Machi 23, 2019.
    Simba SC wataanzia nyumbani Januari 11 dhidi ya J.S. Saoura kabla ya kusafiri kuwafuata AS Vita Januari 18 mjini Kinshasa na Al Ahly Februari 1 mjini Cairo kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza.
    Mzunguko wa pili itaanzia nyumbani Februari 12 dhidi yq Al Ahly mjini Dar es Salaam, kabla ya kusafiri kuwafuata J.S. Saoura nchini Algeria Machi 8 na kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 15. 

    Simba imefuzu tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 15, kufuatia mara ya mwisho kufika hatua hiyo mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Na msimu huu wamefuzu kwa kuitoa Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, wakishinda 3-1 nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini.    
    Wakati mwaka 2003 ilifuzu ikiwa chini ya kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a kipa wa zamani wa Harambee Stars, sasa marehemu, safari hii Simba SC imefuzu ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems mwenye umri wa miaka 53, beki wa zamani wa Ubelgiji aliyechezea klabu za RCS Visé, Standard Liege, K.A.A. Gent, R.F.C. Seraing na ES Troyes AC.
    Na kabla ya Simba, Aussems amefundisha klabu za ES Troyes AC, SS Saint-Louisienne, Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA ya Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C., Shenzhen Ruby, Chengdu Blades, AC Leopards ya Kongo na timu ya taifa ya Nepal.
    Aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba SC, Salum Abdallah 'Try Again' aliiwakilisha klabu yake Cairo  
    Viongozi wa klabu mbalimbali kwenye droo mjini Cairo nchini Misri 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAPANGWA NA AL AHLY, VITA NA TIMU YA ULIMWENGU LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top