• HABARI MPYA

    Wednesday, December 19, 2018

    AZAM FC KUMENYANA NA MADINI JUMAPILI CHAMAZI KOMBE LA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Azam FC Jumapili itaanza kampeni ya kuwania taji la Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kumenyana na Madini FC ya Arusha Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni.
    Azam FC inaanzia raundi ya tatu ya michuano hiyo, sambamba na timu nyingine za Ligi Kuu (TPL), Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL) na timu nyingine za madaraja ya chini zilizoshinda mechi za raundi za awali.
    Msimu uliopita Azam FC ilifungua dimba kwenye raundi hiyo na kuichapa Area C United ya mkoani Dodoma mabao 4-0, yaliyofungwa na kiungo Salmin Hoza, Nahodha Aggrey Morris, mshambuliaji Yahya Zayed na winga Enock Atta-Agyei.

    Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema hawezi kuidharau Madini FC

    Madini inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) imetinga raundi hiyo baada ya kuitoa timu ya Stendi Babati ya mkoani Manyara ikiipa kichapa cha mabao 5-1.
    Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema kwamba hawezi kuidharau timu yoyote atakayokutana nayo kwenye michuano hiyo huku akielezea mipango yake ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji hilo msimu huu.
    “Inaweza ikawa timu ya daraja la tatu, inaweza ikawa daraja la pili, inaweza ikawa timu ya daraja la kwanza au timu ya ligi kuu, hawiezi kubadilisha chochote kwenye maandalizi yako pia, unajaribu kushinda na kufanya kazi kutoka mechi hadi mechi, nilisema unapaswa kumheshimu kila mpinzani unayecheza naye hiyo ina maana kwamba hudharau mpinzani yoyote,” alisema.
    Pluijm anashikilia rekodi ya kuwa kocha pekee aliyeziongoza timu mbili tofauti kuingia fainali ya michuano hiyo, akifanya hivyo msimu 2015/2016 wakati akiipa taji hilo Yanga kwa kuichapa mabao 3-1 timu anayoifundisha sasa na msimu uliopita (2017/2018) akiipeleka Singida United katika hatua hiyo kabla ya kufungwa na Mtibwa Sugar kwenye fainali mabao 2-1.
    Akizungumzia rekodi hiyo, Pluijm alisema anajivunia hilo huku akiweka wazi kuwa michuano hiyo inahitaji bahati na ubora pia wakati mwingine huku akikiri kuwa walikutana na mechi ngumu sana msimu uliopita alipoiongoza Singida United kuingia katika fainali.
    “Lakini msimu huu tunapaswa kuonyesha ubora wetu na kwa matumaini tutafanya vizuri kwenye kombe la ligi pia,” alisema.
    Azam FC itaingia kwenye mchezo huo, ikiwa imeimarisha kikosi chake kwenye idara ya kiungo kwa kumuongeza kiungo mkabaji mzoefu, Stephan Kingue pamoja na mshambuliaji Obrey Chirwa, ambao wameongezwa kwenye usajili wa dirisha dogo.
    Msimu uliopita, Azam FC inayodhaminiwa na vinywaji safi kutoka Kampuni ya Bakhresa Food of Products, juisi za African Fruti na maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, iliishia kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ikitolewa na Mtibwa Sugar kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti 9-8 kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUMENYANA NA MADINI JUMAPILI CHAMAZI KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top