• HABARI MPYA

    Sunday, December 23, 2018

    SIMBA SC WAICHAPA NKANA FC 3-1 NA KUFUZU MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imefanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Nkana FC ya Zambia jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-3, kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza mjini Kitwe Jumamosi iliyopita. 
    Mara ya mwisho Tanzania kuingiza timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa mwaka 2003 na walikuwa hao hao Simba SC waliofika hatua hiyo, wakifuata nyayo za wapinzani wao wa jadi, Yanga SC waliokuwa timu ya kwanza nchini kufikia mafanikio hayo mwaka 1998. 

    Clatous Chama akishangilia mbele ya mashabiki baada ya kufunga bao la tatu 

    Simba SC ililazimika kutoka nyuma kwa bao 1-0 kupata ushindi huo, baada ya wageni, Nkana FC kutangulia kwa bao la Walter Bwalya aliyefunga kwa kichwa dakika ya 17 akimalizia krosi ya Harison Chisala kutoka upande wa kulia.
    Bao hilo lilionekana kuwavuruga Simba SC na kuwapa mwanya Nkana FC kucheza kwa uhuru zaidi uwanjani, lakini kosa la wageni lilikuwa ni kuridhika ba bao hilo, huku wakicheza kwa kujihami.    
    Wachezaji wa Simba wakaamua kuwa wanajaribu kwa mashuti ya mbali na makombora mawili yakawasisimua mashabiki kwanza Erasto Edward Nyoni akigongesha mwamba na baadaye shuti la mshambuliaji Mghana, Emmanuel Okwi likipaa juu kidogo ya lango.
    Lakini shuti la kiungo Jonas Gerald Mkude dakika ya 29 baada ya kupokea pasi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ halikupotea njia, lilimpita kipa Allan Chibwe kama mshale na kuipatia Simba SC bao la kusawazisha.
    Simba SC wakaendelea kulishambulia lango la Nkana FC huku wakirudi haraka kujilinda kila walipopoteza mpira, nidhamu ambayo iliwasaidia kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-1.
    Na hiyo ni baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 45 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki Mghana, Nicholaus Gyan kutoka kulia, zamani mshambuliaji.
    Kipindi cha pili kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J. Aussems alifanya mabadiliko ya mapema katika safu ya ulinzi, akimtoa Mghana, Nicholas Gyan na kumuingiza Mganda Juuko Murshid. 
    Kocha wa Nkana FC, Beston Chambeshi, naye akajibu kwa mabadiliko ya kwenye safu ya ushambuliai, akimtoa Kelvin Kampamba na kumuingiza Chisamba Lungu.
    Simba SC ikapata pigo dakika ya 57 baada ya mfungaji wa bao lake la pili, Kagere kushindwa kuendelea na mchezo kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Hassan Dilunga.
    Nkana nao wakafanya mabadiliko mengine, wakimtoa Ronald Kampamba na kumuingiza Freddy Tshimbenga dakika ya 58 kabla ya kumtoa pia Shadrack Malambo na kumuingiza Festus Mbwewe, wakati Simba nayo baadaye ilimpumzisha Okwi na kumuingiza Shiza Kichuya.
    Mabadiliko hayo yaliinufaisha Simba SC iliyofanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 88 kupitia kwa kiungo wake Mzambia, Clatous Chota Chama aliyemalizia pasi ya Hassan Dilunga.
    Bao hilo liliwazima kabisa Nkana FC walioonekana kucheza kwa kuvizia mikwaju ya penalti pamoja na mshambuliaji wake, Bwalya kupoteza nafasi zaidi ya tatu nzuri za kufunga.
    Nkana inakwenda kumenyana na moja ya timu zilizofuzu hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika Afrika kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo midogo ya CAF. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Nicholas Gyan/Juuko Murshid dk52, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Clotous Chama, Jonas Mkude, John Bocco, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk57 na Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya dk79.
    Nkana FC: Allan Chibwe, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Ben Banh, Richard Ocran, Musa Mayeko, Duncan Otieno, Harrison Chisala, Shadrack Malambo/Festus Mbwewe dk69, Ronald Kampamba/Freddy Tshimbenga dk58, Walter Bwalya na Kelvin Kampamba/Chisamba Lungu dk55.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAICHAPA NKANA FC 3-1 NA KUFUZU MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top