• HABARI MPYA

    Sunday, December 16, 2018

    BAO LA DAKIKA YA MWISHO LA MKONGO MAKAMBO LAIPA YANGA SC USHINDI WA 3-2 DHIDI YA RUVU SHOOTING TAIFA

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Yanga SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting ya Pwani mabao 3-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni ya leo.
    Kwa ushindi huo, timu ya kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inafikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 16, sasa ikiizidi kwa pointi nne Azam FC iliyo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 16 pia.
    Mabingwa watetezi, Simba SC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 27 za mechi 12, wakiwa kwenye mapumziko ya muda mrefu kupewa nafasi ya kushiriki vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, sawa na Mtibwa Sugar waliopo nafasi ya nne kwa pointi zao 23 za mechi 14. 
    Mshambuliaji Mkongo, Heritier Makambo akishangilia baada ya kufunga bao la ushindi

    Kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' akimtoka mchezaji wa Ruvu Shooting leo
    Beki wa Ruvu Shooting, Damas Makwaya akimdhibiti Heritier Makambo wa Yanga

    Damas Makwaya wa Ruvu Shooting akimdhibiti mshambulaiji Amissi Tambwe wa Yanga SC  

    Kikosi cha Ruvu Shooting katika mchezo wa leo Uwanja wa Taifa

    Kikosi cha Yanga SC katika mchezo wa leo Uwanja wa Taira mjini Dar es Salaam

    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Fikirini Yussuf, aliyesaidiwa na Arnold Bugado na Charles Simon hadi mapumziko tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana 1-1.
    Ni Yanga SC waliotangulia kwa bao la Mrundi, Amissi Tambwe aliyeuwahi mpira uliokuwa unakimbiliwa na mshambuliaji mwenzake, Heritier Makambo raia wa DRC ambaye ndiye aliyeingia nao kwenye eneo hilo kuwa kuwapangua walinzi kwa ustadi mkubwa.
    Ruvu Shooting wakasawazisha kupitia kwa mshambuliaji Fullyzulu Maganga aliyemalizia krosi ya Baraka Mtuwi aliyefanikiwa kumpita beki wa kulia wa Yanga, Paulo Godfrey.
    Kipindi cha pili timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na Yanga SC wakawa wa kwanza tena kupata bao, mfungaji kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 78 akimalizia mpira uliorudi baada ya kuokolewa na beki Damas Makwaya kufuatia mpira uliomiminwa na Pius Buswita.
    Kwa mara nyingine, Ruvu Shooting wakasawazisha kwa bao kwa mkwaju wa penalti wa mshambuliaji wake kinara wa mabao, Said Dilunga dakika ya 83 kufuatia Tambwe kuunawa mpira kwenye boksi. 
    Makambo aliye katika msimu wake wa kwanza kwenye soka ya Tanzania akaifungia Yanga bao la tatu na la ushindi dakika ya nne ya muda wa nyongeza baada ya kukamilika kwa dakika 90 za kawaida za mchezo, akimalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib Migomba.
    Na sifa zimuendee beki chipukizi, Paulo Godfrey ‘Boxer’ aliyeingia kishujaa kwenye eneo la hatari la Ruvu Shooting akiwapangua mabeki kabla ya kuangushwa nje kidogo ya boksi na mpira kutengwa kwa pigo la Ajib lililosababisha bao la ushindi.  
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Paulpo Godfrey, Mwinyi Hajji Mngwali/Deus Kaseke dk56, Andrew Vincent/Cleofas Sospeter dk41, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Papy Kabamba Tshishimbi/Pius Buswita dk56, Ibrahim Ajib, Feisal Salum, Heritier Makambo, Amissi Tambwe na Jaffar Mohammed.
    Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Abdul Mpambika, Tumba Swedi, Damas Makwaya, Mau Bofu, Zuberi Dabi, Shaaban Msala, Baraka Mtuwi/Mussa Said dk59, William Patrick/Hamisi Kasanga dk90+2, Fullyzulu Maganga/Alinanuswe Martin dk67 na Said Dilunga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAO LA DAKIKA YA MWISHO LA MKONGO MAKAMBO LAIPA YANGA SC USHINDI WA 3-2 DHIDI YA RUVU SHOOTING TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top