• HABARI MPYA

    Saturday, November 03, 2018

    AMUNIKE AWAREJESHA KIKOSINI TAIFA SARS KICHUYA NA SURE BOY KUIVAA LESOTHO NOVEMBA 18 MASERU, AJIB…

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amemuita kiungo Shiza Ramadhani Kichuya katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na Amunike baada ya kumpuuza katika mechi tatu zilizopita Kichuya, sasa amempa nafasi.
    Jicho la Amunike tu bado halipendezewa na kiungo mwingine mshambuliaji, Ibrahim Ajib Migomba pamoja na kazi nzuri anayoifanya kwa sasa katika klabu yake, Yanga SC japokuwa Taifa Stars itamkosa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta anayetumikia adhabu ya kadi za njano.
    Shiza Kichuya (kulia) amerejeshwa kikosini Taifa Stars kwa ajili mchezo dhidi ya Lesotho

    Ibrahim Ajib (kushoto) bado hajamvutia kocha Mnigeria wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike 

    Lakini winga wa zamani wa Barcelona na Nigeria, Amunike ameimarisha safu yake ya kiungo kwa kumchukua Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuziba pengo la kiungo mwenzake wa Azam FC, Frank Domayo ambaye majeruhi pia.
    Kwa kiasi kikubwa Amunike amerejesha kikosi kilichompa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 mjini Dar es Salaam kikitoka kuchapwa 3-0 mjini Praia na Papa wa Bluu Oktoba 12.
    Makipa ni; Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
    Mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
    Viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum KImenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani.
    Washambuliaji ni Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
    Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMUNIKE AWAREJESHA KIKOSINI TAIFA SARS KICHUYA NA SURE BOY KUIVAA LESOTHO NOVEMBA 18 MASERU, AJIB… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top