• HABARI MPYA

    Saturday, November 24, 2018

    KATABARO AJITOA KUGOMBEA UONGOZI YANGA UCHAGUZI WA JANUARI 13, KEVELA AONDOLEWA KWA WAGOMBEA UENYEKITI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mussa Katabaro amejitoa kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani. 
    Taarifa ya Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake, Malangwe Mchungahela imesema kwamba, Katabaro aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wakati wa Uenyekiti wa Yussuf Manji, hakurejesha fomu, hivyo kwa mujibu wa taratibu amejiengua. 
    Aidha, kamati hiyo imemuondoa Yono Kevela katika orodha ya wagombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Yanga SC na kupitisha wagombea watatu tu, ambao ni Dk. Jonas Benedict Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga.

    Mussa Katabaro hakurejesha fomu ya kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF katika uchaguzi wa Januari 13, mwakani

    Katika orodha hiyo, Kevela amepitishwa kugombea Umakamu pekee pamoja na Titus Eliakim Osoro na Salum Magege Chota.
    Mmiliki huyo wa kampuni maarufu ya minada, Yono Auction Mart Limited aliomba nafasi mbili, Uenyekitina Umakamu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 13 mjini Dar es Salaam maalum kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa wakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016.
    Waliojiuzulu ni aliyekuwa Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF jana kimewapitisha wagombea 16 katika kuwania nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo baada ya kuwaeungua wengine wanne.
    Hao ni Hamad Ally Islam, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvestre Haule, Salim Seif, Shafil Amri, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.
    Walioenguliwa ni Pindu Luhoyo, Mussa Katabaro ambaye hakurudisha fomu, Geoffrey Boniface Mwita na Justin Peter Bisangwa ambao wamekosa sifa za uzofu.
    Baada ya hapo, zoezi litakalofuata ni Kamati ya Uchaguzi kupokea mapingamizi juu ya wagombea hadi Novemba 25 na kuyapitia na kuwafanyia usaili wagombea hadi Novemba 28.
    Novemba 29 Kamati itatangaza matokeo ya usaili na kutaja orodha ya mwisho ya wagombea waliopitishwa, kabla ya kupelekea masuala ya Kimaadili kwa Sekretarieti ya TFF, ambayo itayawasilisha Kamati ya Maadili.
    Desemba 11 hadi 14 Kamati ya Maadili itatangaza uamuzi wa masuala ya Kimaadili iliyoyajadili, kabla ya kutoa fursa ya wagombea walioathirika na zoezi hilo kukata Rufaa na Januari 4 hadi 6 orodha kamili ya mwisho ya wagombea itatolewa baada ya michakato yote tayari kwa kampeni kati ya Januari 8 na 12.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KATABARO AJITOA KUGOMBEA UONGOZI YANGA UCHAGUZI WA JANUARI 13, KEVELA AONDOLEWA KWA WAGOMBEA UENYEKITI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top