• HABARI MPYA

    Sunday, November 18, 2018

    KIPIGO CHA TAIFA STARS LEO MASERU, TFF IMEVUNA ILICHOPANDA

    MWALIMU chipukizi, Oscar Milambo ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati Mnigeria, Emmanuel Amunike anaajiriwa kuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars Agosti mwaka huu.
    Kocha wa zamani wa Taifa Stars na klabu mbalimbali nchini, Salum Madadi aliondolewa katika nafasi hiyo bila sababu za msingi na Milambo pamoja na kuendelea kufundisha timu za vijana, akapewa majukumu hayo pia. 
    Nilimuuliza Rais wa TFF, Wallace Karia kwa nini Milambo mbele ya walimu wote waliobobea nchini hata kama tumeshindwa kuajiri mtaalamu wa kigeni majibu yake yalikuwa; “Oscar Milambo anakaimu. Si ajabu tukasema Oscar ambaye ni kijana ana elimu nzuri na amekwishakwenda kushiriki kozi mbalimbali nje na ni Mtanzania ambaye tunataka tumuwezeshe ili aweze kufanya na ndiyo maana tumempa nafasi hiyo kwa sababu bado ni kijana mdogo na tuna uwezo wa kuendelea kumuwezesha aweze kupata mawazo mapya. Tutakapoona kuna haja kweli ya kuleta mgeni, sawa,”.

    Ni wakati huo huo TFF ilipitisha kanuni ya klabu kusajili na kutumia wachezaji 10 wa kigeni wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara – na huo ndiyo ulikuwa wakati wa kutengeneza programu mbalimbali za maandalizi ya timu za taifa.
    Kwa kumtazama Milambo kwa umri, uwezo na uzoefu wake unaweza kuona alibebeshwa mzigo mzito na matokeo yake tumeanza kuyaona sasa, mwezi mmoja tu tangu ateuliwe Mkurugenzi mpya wa Ufundi, Ammy Ninje.
    Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro ilitolewa mapema tu mechi za kufuzu AFCON U20, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys haikufika fainali ya michuano ya kufuzu CECAFA kufuzu AFCON U17 mwakani na U23 ilifungwa 2-0 kwenye mechi ya kwanza ya kufuzu AFCON U23.
    Mwingiliano wa kalenda za timu za taifa na Ligi Kuu safari hii umekithiri na kusababisha Ligi Kuu kusimama mara kwa mara – inakuwa kama hakukuwa na programu za timu za taifa, hivyo wakati wowote Ligi Kuu inaweza kusimama kwa ajili ya maandalizi ya Taifa Stars.     
    Amunike aliyeteuliwa kuwa kocha wa Taifa Stars amekuja Tanzania kufundisha timu ya kwanza kabisa ya wakubwa ya taifa – amekuja kujifunza kazi hapa.
    Na tunaona anavyojifunza kazi kuanzia namna ya kuishi na wachezaji, kuongoza timu ya taifa na kufundisha pia.
    Mechi nne tu, timu ikitoa sare moja, kufungwa mbili na kushinda moja zimewatosha Watanzania kujiridhisha kwamba Amunike si mtu sahihi kwao, hususan baada ya kipigo cha 1-0 leo kutoka kwa wenyeji, Lesotho mjini Maseru mechi ya Kundi L kufuzu AFCON mwakani nchini Cameroon.  
    Bao lililoizamisha Taifa Stars leo limefungwa na beki wa klabu ya Matlama Maseru, Nkau Lerotholi dakika ya 76 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona kutoka upande wa kulia.  
    Kwa matokeo hayo, sasa timu yoyote kati ya tatu, Lesotho, Tanzania na Cape Verde zinaweza kuungana na vinara wa kundi hilo, Uganda kwenda Cameroon katikati ya mwaka ujao.
    Mamba wa Lesotho wanapanda nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi tano sawa na Tanzania, wakati Cape Verde inashika mkia kwa pointi zake nne.
    Lesotho ikiifunga Cape Verde Machi mwakani itafuzu AFCON hata kama Tanzania itaifungaje Uganda mjini Dar es Salaam kwa sababu ya matokeo ya mechi zilizohusisha timu zilizofungana kwa pointi.
    Cape Verde nayo itafuzu ikiifunga Lesotho na Tanzania ikalazimishwa sare ya Uganda. Taifa Stars inaweza kufuzu iwapo itaifunga Uganda na Cape Verde ikashinda au kutoa sare na Lesotho katika mechi za mwisho.   
    Dalili za Taifa Stars kupoteza mechi ya leo zilianza kuonekana mapema tu kutokana na kuzidiwa na wenyeji na kuanza kukoswa mabao ya wazi mapema.
    Lakini upangwaji wa kikosi na mfumo wa kujihami wa kocha Amunike aliyewaacha benchi wachezaji wazoefu akiwemo mshambuliaji John Raphael Bocco aliyepewa nafasi kubwa ya kuanza, navyo vilichangia.
    Aidha, kuwachezesha wachezaji nje ya nafasi zao nako kuliipa mzigo mzito timu leo kupata matokeo mazuri iliyotahitaji.
    Kweli uwezo wa Tanzania kama nchi kisoka, lakini Amunike naye amewaonyesha wananchi uwezo wake ni wa kiasi gani.
    Na nikakumbuka majibu ya Karia nilipomuuliza Agosti mwaka huu kipi kimewashawishi kumchukua kocha Amunike?
    “Sisi tunatafuta mtu ambaye tunahisi kwamba atatufikisha kule ambako tunastahili na ndiyo tumeona kwamba yeye ndiye anatufaa, inawezekana wakawa wapo wengi, lakini kwa jicho letu sisi na mazungumzo, ndiyo ambaye ameelekea na tumekubaliana naye na ni jambo ambalo halina mjadala kwa Emmanuel Amunike na malengo yetu ambayo tunataka ni kuwa na sisi hapa,”.
    TFF ilicheza kamari kumpa timu Amunike, kwa sababu hajawahi kufundisha timu yoyote ya taifa ya wakubwa hapo kabla na ametumia fursa hii kujifunza na labda baadaye atakuwa mwalimu mzuri baada ya huu uzoefu anaoupitia.
    TFF chini ya Rais Karia inachukulia mambo mengi kwa wepesi mno na ndiyo maana Mtendaji Mkuu wa shirikisho hilo ni Wilfred Kidau na kwa ujumla mambo yaanakwenda kama yanavyokwenda.
    TFF ingezingatia umuhimu wa mwalimu mzoefu ambao Uganda waliutazama wakati wanatafuta kocha hadi kumpata Mfaransa, Sebastien Desabre, aliyefanikiwa kuwapeleka AFCON ya mwakani labda hadithi zingekuwa tofauti leo.
    Na kwa kifupi tunaweza kusema matokeo ya leo Maseru, TFF imevuna ilichopanda. Kutofuata misingi ya kitaalamu, ujuaji na kuchukulia mambo kwa wepesi. Poleni Watanzania wenzangu. Tusikate tamaa, tuendelee kumuomba Mungu na kuambiana ukweli. Ipo siku.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPIGO CHA TAIFA STARS LEO MASERU, TFF IMEVUNA ILICHOPANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top