• HABARI MPYA

    Friday, November 10, 2017

    YANGA ‘WAMLIMA MEMO’ NGOMA, KAMUSOKO NA TAMBWE NAO HALI BADO TETE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imemuandikia barua mshambuliaji wake, Donald Dombo Ngoma kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo cha kuchelewa kurudi baada ya ruhusa ya kwenda kwao kwa matatizo ya kifamilia.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba wamemuandikia barua hiyo Ngoma kwa kuchelewa kurudi kazini baada ya ruhusa maalum.
    “Barua itamfikia huko huko aliko (Zimbabwe), ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo hiki,”amesema Mkwasa.
    Donald Ngoma (kushoto) ameandikiwa barua ya kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu Yanga 

    Inafahamika Ngoma ni majeruhi kwa sasa na alikwenda kwao Zimbabwe kushughulikia matatizo ya kifamilia baada ya ruhusa ya kocha Mkuu, Mzambia, George Lwandamina.
    Lakini inaelezwa Ngoma hakuwasiliana na ofisi ya Katibu Mkuu wa klabu, Mkwasa baada ya ruhusa ya kocha Lwandamina na mbaya zaidi amepitisha muda wa ruhusa yake.
    Ngoma aliomba ruhusa ya wiki moja, lakini sasa inakwenda wiki ya tatu hajarejea kazini na ni kwa sababu hiyo Mkwasa ameamua kumuandikia barua, ambayo hatua zaidi zitajulikana baada ya majibu yake.
    Kwa msimu wa pili, Ngoma amekuwa mchezaji ambaye hana mchango wa kutosha ndani ya kikosi cha Yanga kutokana na kusumbuliwa na maumivu.
    Ikijua kabisa bado anasumbuliwa na maumivu, Yanga ilicheza kamari kuwa kumpa mkataba mpya mnono Mzimbabwe huyo Julai mwaka huu – hatua ambayo bila shaka wamekwishaanza kuijutia, kwani bado Ngoma hajawa imara kuisaidia klabu. 
    Katika hatua nyingine, wachezaji wengine majeruhi wa muda mrefu, kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe wameshindwa kuanza mazoezi kwa sababu bado wanasikia maumivu.
    Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema timu imefanya mazoezi leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, lakini Kamusoko na Tambwe hawakuweza kufanya.
    “Kwa kweli siwezi kujua wataanza lini, maana wamekuwa wakitibiwa vizuri tu, lakini kila wakijaribu kuanza mazoezi, wanasema wanasikia maumivu, wanarudi kwenye matibau tena,”amesema Hafidh.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA ‘WAMLIMA MEMO’ NGOMA, KAMUSOKO NA TAMBWE NAO HALI BADO TETE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top