• HABARI MPYA

    Wednesday, March 22, 2017

    HAWA NDIYO MC ALGER, WAPINZANI WAPYA WA YANGA AFRIKA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa, vigogo wa Tanzania, Yanga SC watamenyana na MC Alger ya Algeria katika mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya droo iliyopangwa jana mjini Cairo, Misri.
    Timu zilizotolewa Ligi ya Mabingwa zitamenyana na zilizosonga mbele Kombe la Shirikisho katika mechi za nyumbani na ugenini kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani.
    Mechi za kwanza zinatarajiwa kucheza wikiendi ya Aprili 7 hadi 9 na marudiano yanatarajiwa kuwa wikiendi ya Aprili 14 hadi 16, mwaka huu.
    Yanga SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanacio Jumamosi Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia.
    Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inatolewa kwa mabao ya ugenini, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

    IJUE MC ALGER...
    Inaitwa Mouloudia Club d'Alger, ama MC Alger au MCA kwa kifupi, ni klabu ya soka ya Algeria yenye maskani yake Jijini Algiers, ambayo inacheza mechi Ligi Kuu ya Algerian, ijulikanayo kama Ligue Professionnelle 1.
    Ilianzishwa mwaka 1921 kama Mouloudia Chaàbia d'Alger, na baadaye ikawa inajulikana kama Mouloudia Petroliers d'Alger kuanzia mwaka 1977 hadi 1986 kabla ya kubadili tena jina na kuwa Mouloudia Club d'Alger  mwaka 1986. 
    Ni timu ambayo inatumia jezi za rangi ya nyekundu na kijani na inacheza mechi zake Uwanja wa Omar Hamadi.
    Hiyo ndiyo klabu ya kwanza ya Algeria kushinda kushinda taji la Afrika, walipofanikiwa kubeba Kombe la Klabu Bingwa barani mwaka 1976. 
    Ni moja ya timu zenye mafanikio makubwa nchini Algeria ikiwa imetwaa mataji saba ya Ligi, ikishika nafasi ya pili kutwaa mara nyingi baada ya JS Kabylie, na vikombe vya nyumbani saba, ikishika nafasi ya tatu kutwaa mara nyingi baada ya USM Alger na ES Setif.

    ILIVYOANZISHWA...
    Mwaka 1921, kikundi cha vijana majirani kutoka Casbah na Bab El Oued waliungana pamoja kuanzisha klabu ya kwanza ya Kiislamu katika Algeria ya kikoloni.
    Kundi hilo liliongozwa na Hamoud Aouf, ambaye alikuwa muunganishi wa makundi hayo na Agosti 7, mwaka 1921, klabu hiyo ilianzishwa rasmi katika sebule ya mgahawa wa Benachere. 
    Kwa sababu timu hiyo ilianzishwa katika tarehe za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W.), timu hiyo ikapewa jina Mouloudia Club d'Alger na kuchagua rangi za kijani na nyekundu kwa ajili ya jezi zao. 
    Kijani inawakilisha matumaini ya Waalgeria na rangi ya kitamaduni ya Kiislamu, wakati nyekundu ni kwa ajili ya mapenzi kwa nchi yao.
    Mwaka 1976, MC Alger ikafuzu Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya kutwaa ubingwa wa Algeria msimu wa 1974–1975.
    Walifanikiwa kufika fainali baada ya kuzifunga Al-Ahly Benghazi ya Libya, Al-Ahly ya Misri, Luo Union ya Kenya na Enugu Rangers ya Nigeria.
    Katika fainali, wakakutana na Hafia Conakry ya Guinea, na kwenye mechi ya kwanza mjini Conakry, MC Alger ikafungwa mabao 3–0 na kuekelea kwenye mchezo mgumu wa marudiano. 
    Pamoja na hayo, kwenye mchezo wa marudiano wakafanikiwa kufunga mabao matatu, huku Omar Betrouni akifunga mawili na lingine Zoubir Bachi, hivyo mchezo kuhamia kwenye mapigo ya penalti na Waalgeria hao wakashinda 4–1 na kutwaa ubingwa wa Afrika
    Hawa ni mabingwa wa Ligi ya Algeria, League 1 mara saba katika miaka ya 1972, 1975, 1976, 1978, 1979, 1999 na 2010 na ni washindi wa Kombe la Algeria mara nane, miaka ya 1971, 1973, 1976, 1983, 2006, 2007, 2014 na 2016.
    Pia ni washuindi wa Super Cup yab Algeria mara tatu katika miaka ya 2006, 2007, 2014 na washindi mara mbili wa Kombe la Ligi la Algeria miaka ya 1998, 1999.
    Matokeo yao mazuri ya mwisho ya MC Alger katika michuano ya Afrika ni kufika Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1980, wakati mwaka 2011 ilikomea hatua ya makundi. Mwaka jana, kama 2008 na 2007 ilitolewa hatua ya 32 Bora tu ya Kombe la Shirikisho.
    Je, Yanga itaweza kuupanda mlima huu wa Algeria ili kudondokea hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho?
    Bila shaka muda ukifika utatoa majibu.  Mechi za kwanza kati ya Aprili 7 na 9 na marudiano Aprili 14 na 16, mwaka huu. Kila la heri Yanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAWA NDIYO MC ALGER, WAPINZANI WAPYA WA YANGA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top