• HABARI MPYA

  Wednesday, June 01, 2016

  JUMAMOSI NI HATIMA YETU, TWENDENI TUKAISAPOTI TAIFA STARS YETU

  WAKATI natazama mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Jumapili Uwanja wa Kasarani, Nairobi, Kenya, kupitia Televisheni ya Azam TV, 
  kuna jambo lilinifurahisha kidogo.
  Ni pale mtangazaji wa KBC ya Kenya ambayo ilishirikiana na Azam TV kurusha mchezo huo aliposema eti Tanzania na Kenya zote zimekwishatolewa kwenye 
  mbio za kuwania tiketi ya Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Kenya waliopo Kundi E, wanashika mkia baada ya kuambulia pointi moja katika mechi nne wakati Guinea Bissau inagongoza kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Kongo na Zambia zenye pointi sita kila moja. 

  Tanzania wapo Kundi G ambako pia wanashika mkia kwa pointi yao moja baada ya kucheza mechi mbili, wakifungwa ugenini na Misri 3-0 na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria nyumbani, Misri inaongoza kundi hilo kwa pointi zake saba baada ya kucheza mechi tatu sawa na Nigeria yenye pointi mbili.
  Zote, Misri na Nigeria zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina mechi mbili – kwanza Jumamosi na Misri nyumbani na baadaye Septemba na Nigeria ugenini.
  Iwapo Tanzania watashinda mechi zote mbili za mwisho watamaliza na pointi saba sawa na Misri, hivyo timu ya kufuzu AFCON ya mwakani kutoka Kundi G itapatikana kwa wastani wa mabao.
  Hii inamaanisha kwamba mtangazaji wa KBC aliwaongopea watazamaji kwake tu kwa uvivu wa kufikiria, akawalisha maneno ya uongo.
  Haikuwa sahihi kusema Kenya na Tanzania zimekwishapoteza nafasi ya kwenda AFCON – labda angeizungumzia nchi yake tu na nafasi yao.
  Tanzania bado ina nafasi nzuri tu ya kwenda AFCON, lakini ni iwapo itashinda mechi zake mbili zilizobaki.
  Mchezo wa Jumamosi ni muhimu kwa Stars kushinda ili kuendelea kuweka hai matumaini ya AFCON na hatimaye kwenda Nigeria kwa nguvu zaidi katika mchezo wa mwisho.
  Na hapo ndipo unapoonekana umuhimu wa kuhamasishana baina yetu Watanzania ili tujitokeze kwa wingi Jumamosi Uwanja wa Taifa kuwatia ngugu vijana wetu washinde mchezo huo.
  Nigeria ndiyo ambayo imekwishapoteza nafasi ya kwenda AFCON, ikiathiriwa na kujitoa kwa Chad katika kundi hilo, hivyo kubaki timu tatu.
  Taifa Stars na Mafarao ndiyo wanawania kuwa timu ya Kundi G itakayofuzu AFCON ya mwakani na wazi mchezo wa Jumamosi utakuwa na upinzani mkali.
  Misri wanahitaji sare tu siku hiyo ili kujihakikishia kwenda AFCON na ikitokea wakafungwa maana yake watalazimika kusubiri matokeo ya mchezo wa mwisho kati ya Nigeria na Tanzania ili kujua mustakabali wao.
  Tuondoe mawazo tunakwenda kucheza na Misri katika moja ya mechi za kukamilisha ratiba, la hasha bali tunakwenda kupigania tiketi ya AFCON.
  Na kama inavyoonekana katika siku za karibuni Taifa Stars imeendelea kuimarika chini ya kocha mzalendo Charles Boniface Mkwasa, aliyechukua nafasi ya Mholanzi, Mart Noooij
  Shime Watanzania, tujitokeze kwa wingi Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwenda kuishangailia Taifa Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwani nafasi ya AFCON bado tunayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JUMAMOSI NI HATIMA YETU, TWENDENI TUKAISAPOTI TAIFA STARS YETU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top