• HABARI MPYA

    Wednesday, March 26, 2014

    YANGA SC WAJIFUNZE KUWAPENDA NA KUWASAPOTI WACHEZAJI WAO KWA SHIDA NA RAHA

    GHANA ilikaribia kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kucheza Nusu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
    Lakini ilishindwa kuweka rekodi hiyo baada ya mshambuliaji wake nyota na tegemeo wakati huo, Asamoah Gyan kukosa penalti dakika za majeruhi dhidi ya Uruguay katika mchezo wa Robo Fainali.
    Penalti hiyo hiyo ilitolewa baada ya mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez kujigeuza kipa na kuokoa kwa mkono mpira uliokuwa unaelekea nyavuni, lakini Gyan akaenda kugongesha mwamba na kufanya mshindi wa mchezo huo apatikane kwa sheria ya mikwaju ya penalti.

    Hakika Gyana aliwaumiza siyo tu Waghana, bali na Waafrika kwa ujumla kwa kukosa penalti ile, lakini kwa sababu benchi la Ufundi la Black Stars na wachezaji wenzake walijua hilo ni jambo la kawaida katika mchezo, walikuwa wa kwanza kumsamehe.
    Hata FA ya Ghana ilimsamehe na Waghana pia wakamsamehe, na bila shaka hata sisi Waafrika wengine tulimsamehe.
    Alisamehewa kwa sababu ilichukuliwa ni bahati mbaya na rekodi yake ya kufunga mabao mazuri yakiwemo ya penalti kabla ya siku hiyo, ilimfanya aendelee kuaminiwa na kuheshimiwa.   
    Ni Gyan ambaye alifunga kwa penalti dakika ya 85 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Serbia Kombe la Dunia 2010, Ghana ikishinda 1–0. 
    Alifunga pia katika mchezo wa pili wa Ghana kwenye fainali hizo kwa penalti dakika ya 26 kusawazisha na kuipa Black Stars sare ya 1–1 na Australia na katika Hatua ya 16 Bora, katika mechi dhidi ya Marekani, alifunga katika muda wa nyongeza kuipa Ghana ushindi wa kwenda Robo Fainali na kuweka rekodi ya kuwa timu ya tatu barani kufika hatua hiyo, baada ya Cameroon na Senegal.
    Na pamoja na kukosa penalti katika Robo dhidi ya Uruguay, kwenye matuta ya kusaka mshindi, Gyan alipewa tena penalti na akafunga, ingawa Ghana ilitolewa kwa 4-2.
    Mwaka jana katika Kombe la Shirikisho, Azam FC ilikaribia kuingia Nane Bora kama si John Bocco ‘Adebayor’ kukosa penalti mjini Rabat dhidi ya wenyeji AS FAR Rabat zikiwa zimesalia dakika nane mchezo kwisha.
    Kabla ya kupewa penalti hiyo, Bocco ndiye aliyekuwa anaaminiwa zaidi katika kupiga mikwaju hiyo ndani ya Azam- lakini siku hiyo akaingia kwenye orodha ya wachezaji wengine wazuri waliowahi kukosa penalti, kama Zinadine Zidane, Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Hussein Marsha, Hamisi Gaga, Luis Suarez na wengine.
    Katika mechi ya Ligi Kuu ya Bara Jumatano ya wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji wa Yanga SC, Hamisi Kiiza alikosa penalti timu yake ikilazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC baada ya kipa Aishi Manula kupangua.
    Baada ya mchezo huo, Kiiza alijikuta anatoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo akiwa anabubujikwa machozi, kutokana na kutukanwa sana na wapambe wa viongozi wa timu hiyo.
    Lakini wiki moja kabla, Yanga SC ilitolewa na Al Ahly ya Misri mjini Alexandria kwa penalti 4-3 katika Ligi ya Mabingwa Afrika Raundi ya Kwanza kufuatia sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Yanga walipoteza penalti tatu kupitia kwa Oscar Joshua, Said Bahanuzi na Mbuyu Twite siku hiyo Hamisi Kiiza alitolewa dakika za mwishoni.
    Baada ya Yanga kutolewa, mashabiki wa timu hiyo wakawa wanamlaumu kocha Mholanzi, Hans van der Pluijim kwa kuwatoa wapiga penalti kama Hamisi Kiiza na kuacha wachezaji ambao hawajui kupiga penalti.
    Walikuwa sahihi kusema hivyo, kwa sababu siku zote Kiiza amekuwa mmoja wa wapiga penalti wazuri ndani ya Yanga SC, lakini baada ya kukosa dhidi ya Azam, akageuziwa kibao na kutukanwa, tena akiambiwa aliikimbilia kazi ambayo ilitakiwa kufanywa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.  
    Huyu Cannavaro ambaye sasa anaonekana lulu baada ya kufunga bao pekee la ushindi katika mchezo dhidi ya Ahly Dar es Salaam, siku zote amekuwa akionekana takataka na kila baya amekuwa akiambiwa yeye na alikuwa wa kutemwa tangu msimu uliopita.
    Cannavaro amekwishazomewa sana na Yanga SC hadi kuimbiwa ‘toa huyoo’- lakini leo ni mfalme. Ila, Yanga SC wanapaswa kujua, Cannavaro ni binadamu na mpira wa miguu ni mchezo wa makosa-na makosa yanafanywa na wachezaji, basi iko siku atakosea, je watamvumilia?
    Yanga SC wanapaswa kuwajua vyema wachezaji wao, kuwatambua na kuwaheshimu kwa vipindi tofauti wanavyopitia- kwa kifupi wajifunze kuwa pamoja na wachezaji wao wakati wa furaha na simanzi.
    Mchezaji anayekosa penalti, ni ambaye angefunga angekimbia kushangilia. Unadhani anakuwa katika hali gani anapokosa? Yanga SC wajifunze kuwapenda wachezaji wao, kuwasapoti wakati wote hata wanapokosea, kwani hayo ni mambo ya kawaida katika mchezo. Jumatano njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAJIFUNZE KUWAPENDA NA KUWASAPOTI WACHEZAJI WAO KWA SHIDA NA RAHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top