• HABARI MPYA

    Sunday, March 23, 2014

    TIMU ZA MAJESHI YETU ZINATIA AIBU LIGI KUU, TATIZO LIKO WAPI?

    UKITAZAMA msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kuna timu za majeshi mbalimbali ya nchi yetu, ya ulinzi na usalama zipatazo sita.
    Jeshi la Kujennga Taifa (JKT) pekee lina timu nne, ambazo ni JKT Ruvu, JKT Oljoro, JKT Mgambo na Ruvu Shooting, wakati Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lina timu moja, Rhino Rangers na Magereza wana timu moja, Prisons. 
    Jeshi la Polisi nalo limekuwa likipata wawakilishi katika Ligi Kuu mara kadhaa kupitia timu zao za Morogoro na Dodoma.
    Jeshi ni taasisi kubwa na ni imani ya wengi huko wachezaji wanaajiriwa, wanalipwa mishahara na kwa ujumla wanalelewa vizuri.

    Na inafahamika kwa wanamichezo, mara nyingi jeshini hawana majukumu ya ziada, zaidi ya kuelekeza nguvu zao kwenye michezo.
    Inaaminika, wachezaji wa timu za jeshi wanapata muda mzuri wa kufanya mazoezi, lishe nzuri na wakati wote wanakuwa wapo kambini.
    Pamoja na yote hayo, ukifuatilia mwenendo wa timu hizo katika Ligi Kuu hauendani na hali halisi ya mazingira yake, ambayo wengi tunayajua.
    Ukweli ni kwamba, ushiriki wa timu za majeshi katika Ligi Kuu si mzuri na zaidi kuna timu mbili zilizodumu kwa muda mrefu kwenye ligi hiyo, JKT Ruvu na Ruvu Shooting, hizo zimekuwa kama zinacheza ligi hiyo ili zishuke tu, lakini haziashirii kuwa na malengo ya ziada.
    Katika ligi ya sasa inayoendelea, timu tano za jeshi zinapambana kuepuka kushuka Daraja zikiwa katika nafasi sita za chini pamoja na Ashanti United, tena zikiwa zinapishana kidogo tu kwa pointi.
    Ruvu Shooting ndiyo timu iliyo juu ya timu zote za juu katika Ligi Kuu, ipo nafasi ya sita kwa pointi zake 28, inaizidi kwa pointi tatu tu JKT Ruvu iliyo nafasi ya tisa. Prisons yenye pointi 22 ni ya 10, Mgambo JKT pointi 18, sawa na Ashanti, JKT Oljoro pointi 15 na Rhino Rangers inashika mkia kwa pointi zake 13.
    Lakini huko chini, kuna timu nyingine za majeshi zinapigania kupanda Ligi Kuu msimu ujao na zitapanda- japokuwa aina ya ushiriki wake haitarajiwi kubadilika na kwa timu za Polisi zenyewe huwa zinakuja na kuondoka msimu ule ule.
    Inakumbukwa siku za mwanzoni za ujio wa Prisons na JKT Ruvu katika Ligi Kuu, zilikuwa timu tishio na shindani katika ubingwa wa Ligi Kuu. 
    Wapumzike kwa amani Meja Jackson Lema aliyekuwa JKT Ruvu na Talib Talib aliyekuwa Prisons- wawili hao wakiwa viongozi wa timu hizo walizifanya ziwe tishio kweli nchini.
    Lakini inastaajabisha leo makali ya timu hizo yalipopotolea hadi zimekuwa za kupambana kuepuka kushuka daraja. Nini haswa kinakosekana katika timu za majeshi?
    Kuna wakati tulikuwa tunalaani ligi yetu kuwa na timu nyingi za mtaani, ambazo hazijiwezi kifedha inachangia kuwa dhaifu, hivyo kushindwa kutoa ushindani kwa sababu kadha wa kadhaa.
    Zinauza mechi, au hazina uwezo kwa sababu hazina fedha za kufanya maandalizi ya kucheza Ligi Kuu, hayo ndiyo yamekuwa mawazo ya wengi juu ya timu aina ya Toto African na Manyema Rangers. 
    Kwa sasa ligi yetu inashirikisha timu zenye msimamo tupu, labda unaweza kuitilia shaka Ashanti United pekee, lakini nayo ina udhamini unaowawezesha kupata fedha za kujikimu kutoka kampuni ya Bakhresa Group.
    Coastal Union ina wafadhili akiwemo Nassor Bin Slum, haina matatizo wakati Mtibwa Sugar na Kagera Sugar nazo hazina shida zinamilikiwa na viwanda vya sukari. Mbeya City inamilikiwa na Halmshauri ya Jiji la Mbeya, haina matatizo na imeonyesha usindani msimu huu ikicheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.
    Zaidi ya hapo, timu nyingine za Ligi Kuu ni Simba, Yanga na Azam ambazo zimekuwa zikishindania ubingwa kwa misimu minne sasa. Wazi sasa tuna ligi ya timu zisizo njaa, lakini ajabu timu za majeshi ni dhaifu.
    Rekodi ya kufungwa mabao mengi hadi sasa katika Ligi Kuu msimu huu inashikiliwa na timu za majeshi, Ruvu Shooting walifungwa 7-0 na Yanga na Mgambo JKT walifungwa 7-1 na Simba SC. Hii ni fedheha kwa kweli kwa majeshi yetu.
    Baadhi ya nchi za wenzetu timu za majeshi ndiyo wawakilishi imara wa mataifa yao katika michuano ya Afrika, lakini kwetu timu za majeshi ndiyo vibonde. Tatizo liko wapi?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TIMU ZA MAJESHI YETU ZINATIA AIBU LIGI KUU, TATIZO LIKO WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top