• HABARI MPYA

    Wednesday, March 26, 2014

    SEIF MAGARI WA YANGA SC KUBURUZWA MAHAKAMANI

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ amepewa siku saba kuanzia Machi 21, mwaka huu awe amekwishalipa fedha za awali walizopewa kwa ajili ya kuuza haki za matangazo ya Televisheni kwa mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa dhidi yao na Al Ahly ya Misri, vinginevyo ataburuzwa Mahakamani.
    Kwa mujibu wa barua ya Mwakilishi wa kampuni ya MGB, Francis Gaitho aliyeingia Mkataba na Yanga SC, ambayo BIN ZUBEIRY imeipata nakala yake, Seif Magari ametuhumiwa kuwa ndiye aliyekwamisha mpango wa mechi hiyo kurushwa.
    Wanataka kukuburuza mahakamani; Seif Magari kulia akiwa na kiongozi wa zamani wa Yanga SC na mwanachama wa siku nyingi wa klabu hiyo, Abdul Sauko kushoto

    “Unatakiwa kuwa umejibu ndani ya siku saba za kazi, ukishindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitafuata,”imesema barua ya Gaitho.
    Yanga SC ilitangaza kuingia Mkataba wa dola za KImarekani 90,000 na kampuni hiyo kwa ajili ya kuonyesha mechi hiyo nchi za Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati, lakini nakala ya Mkataba ambayo BIN ZUBEIRY inayo wameandikishana dola 55,000 tu na ikapewa malipo ya awali dola za Kimarekani 16,500.
    Mwakilishi wa kampuni ya MGB, Francis Gaitho aliwalalamikia Yanga SC kukwamisha zoezi la kurusha mechi hiyo, akidai waliwafukuza uwanjani kampuni ya Star TV na kamera zao waliokwenda kufanya zoezi hilo. 
    Gaitho alisema baada ya kusaini Mkataba na Yanga, waliwalipa fedha za awali kutoka kwenye akaunti yao nchini Misri kwenda kwenye akaunti ya klabu hiyo Tanzania.
    Hata hivyo, akasema timu ya watu wa utayarishaji waliotakiwa kuja kurekodi mchezo huo ilishindwa kufika nchini kwa wakati kutoka Cairo, hivyo wakalazimika kutafuta kampuni ya hapa Tanzania kufanya kazi hiyo na Star TV ikabahatika kupata tenda hiyo.
    Gaitho akasema kwamba licha ya barua ya Ubalozi wa Misri kwamba MGB italipa malipo yaliyobaki baada ya mechi na kudhaminiwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Yanga SC waligoma mechi hiyo kurekodiwa. 
    “Wakati tulipofikia mwafaka na kukubaliana mechi irekodiwe, bahati mbaya Star TV walikuwa tayari wamekwishaondoka uwanjani na muda ulikuwa umeenda,”alisema Gaitho. 
    Akalaani kwamba kukwama kuonyeshwa kwa mechi hiyo hakujawaathiri Watanzania pekee, bali na Wamisri pia katika wakati huu ambao nchi zinajaribu kujenga uhusiano mzuri baina yao, na hususan kwenye soka zama hizi ambazo wachezaji wananunuliwa.
    “Ilikuwa ni fursa nzuri kwa wachezaji wa Tanzania kuonyesha vipaji vyao Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, na pengine wangeweza kuzivutia klabu za nje zikawasilisha ofa ya kuwanunua katika klabu yao na kusaidia kukuza pato la klabu yao,”alisema.
    Juhudi za kumpata Seif mwenyewe kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, ingawa zinaendelea.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SEIF MAGARI WA YANGA SC KUBURUZWA MAHAKAMANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top