• HABARI MPYA

    Sunday, March 30, 2014

    MASHALI AMSHINDA KASEBA, ILA NGUMI ZILIPIGWA HASWA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    BONDIA Thomas Mashali amefanikiwa kutwaa taji la WBO uzito wa Light Heavy baada ya kumshinda kwa pointi Japhet Kaseba usiku huu kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba, Temeke mjini Dar es Salaam.
    Majaji wote watatu walimpa ushindi bondia wa Manzese wa pointi 97-93 dhidi ya mbabe wa Kinondoni baada ya pambano hilo la raundi la 10, ambalo lilimalizika bila mtu kuanguka chini hata kwa sekunde wala kuhesabiwa kwa kuleweshwa ngumi.
    Mshindi juu; Thomas Mashali akiwa amebebwa juu na mashabiki wake baada ya kutangazwa mshindi dhidi ya Japhet Kaseba

    Kaseba aliyepanda ulingoni na mbwembwe nyingi, alianza vibaya katika raundi mbili za kwanza kabla ya kusimama imara katika raundi ya tatu na kumsukumia makonde mazito mpinzani wake.
    Kaseba alirudi kwa kujiamini raundi ya nne na kumtandika mpinzani wake katika raundi yote hiyo. Hata hivyo, Mashali alizinduka raundi ya tano na kumdhibiti mpinzani wake, akianza kurusha ngumi za mbali na kuhama upande haraka.
    Raundi ya sita, Kaseba aliingia na maarifa ya kupiga na kukumbatia hatimaye kufanikiwa kumpunguza kasi Mashali.
    Kaseba alifanya vizuri katika raundi ya saba na ya nane, lakini Mashali akazinduka raundi ya tisa na kumalizia ya 10 pia vizuri.
    Thomas Mashali kulia akipambana na Japhet Kaseba kushoto

    Japokuwa hata matokeo yangetangazwa sare kusingekuwa na malalamiko, lakini Japhet aliridhia uamuzi wa majaji na kumkumbatia Mashali baada ya pambano.
    Pamoja na ushindi, lakini Mashali hakucheza katika kiwango chake kiasi cha kumaliza raundi 10 na rasta mwenzake huyo ambaye kwa sasa anacheza ngumi kwa kulazimisha tu, kwani uwezo uliofanya akaitwa ‘Champ’ umekwishamkimbia. 
    Bingwa na mataji; Thomas Mashali akiwa na mikanda yake baada ya kumshinda Japhet Kaseba
    Katika mapambano ya utangulizi, Alan Kamote alimshinda kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Karage Suba na kutwaa ubingwa wa UBO uzito wa Light, pambano kati ya Freddy Sayuni na Rajab Maoja lilivunjika raundi ya nne baada ya Maoja kuchanika na kushindwa kuendelea kugombea ubingwa wa PST.  
    Said Mundi alimpiga Jumanne Mohamed kwa pointi pambano la uzito wa bantam, Issa Nampepeche alimpiga kwa pointi Zuberi Kitandula uzito wa bantam pambano lisilo la ubingwa, Saidi Chaku alitoka sare na Jocky Hamisi pambano la Feather lisilo la ubingwa na Majid Said alimpiga kwa pointi Frank Zaga uzito wa bantam pambano lisilo la ubingwa pia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASHALI AMSHINDA KASEBA, ILA NGUMI ZILIPIGWA HASWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top