• HABARI MPYA

    Sunday, March 23, 2014

    AZAM YAITOROKA YANGA, YAZIDI KUUKARIBIA UBINGWA

    Na Saada Akida, Dar es Salaam
    AZAM FC imepiga hatua kuikimbia Yanga SC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia kuifunga JKT Oljoro bao 1-0 jioni hii Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yanaifanya Azam FC itimize pointi 47 baada ya kucheza mechi 21, ikiwazidi mabingwa watetezi, Yanga SC kwa pointi nne ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.
    Shujaa; John Bocco 'Adebayor' katikati ameifungia bao pekee Azam FC jioni ya leo ikizidi kuusogelea ubingwa

    Shujaa wa Azam FC hii leo alikuwa ni John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao hilo peke dakika ya 71 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kinda Kevin Friday. 
    Azam FC ilipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Brian Umony dakika ya tisa, Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 11, Kipre Tchetche dakika ya 13, John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 39.
    JKT Oljoro ilifika kwenye lango la Azam mara moja tu dakika ya 33, baada ya pasi ya Iddi Swalehe kumfikia Shijja Mkina, lakini shuti lake likadakwa na kipa Aishi Salum Manula.  
    Kipindi cha pili, kocha Mcameroon wa Azam FC, Joseph Marius Omog alianza na mabadiliko, akimpumzisha mshambuliahji Mganda, Brian Umony dakika ya 49 ambaye bafasi yake ilichukuliwa na kinda Kevin Friday.
    Omog aliwapumzisha pia Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 58 na nafasi yake kuingia Mudathir Yahya, wakati Brison Raphael alimpisha Gaudence Mwaikimba dakika ya 73.  
    Kikosi cha Azam FC; Aishi Manula, Himid Mao, Gadiel Michael, Said Mourad, David Mwantika, Brison Raphael/Gaudence Mwaikimba dk73, Khamis Mcha ‘Vialli’/Mudathir Yahya dk58, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Brian Umony/Kevin Friday dk49, John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche.
    JKT Oljoro; Mohamed Ally, Naplo Zuberi, Ally Hamza, Nurdin Suleiman, Shaibu Nayopa, Jacob Raymond, Hamisi Maulid/Babu Ally dk68, Amir Omary, Shija Mkinna/Juma Mohammed dk62, Yussuf Machogore na Iddi Swalehe.
    Katika mechi nyingine, Simba SC imefungwa 1-0 na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la Hamad Juma dakika ya 44, Ruvu Shooting imeifunga 2-0 Ashanti United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani mabao ya Elias Maguri dakika za sita na 63 wakati Mgambo JKT imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAITOROKA YANGA, YAZIDI KUUKARIBIA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top