• HABARI MPYA

    Friday, March 21, 2014

    MAPATO YANGA NA AZAM YAIKWAMA TFF, YATANGAZA KUUNDA KIKOSI KAZI KUSHUGHULIKIA TIKETI ZA ELEKTRONIKI

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    TOFAUTI na ilivyo kawaida ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza mapato siku moja baada ya mechi zinazozihusu klabu zenye mashabiki wengi, Simba na Yanga- hadi leo shirikisho hilo halijataja mapato ya mechi ya juzi kati ya Yanga na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
    Ofisa Habari  na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo ambaye hutuma taarifa hizo, ameshindwa kuorodhesha taarifa ya mapato ya mechi hiyo ya Ligi Kuu iliyoisha kwa sare ya 1-1 katika taarifa zake za jana na leo.
    Mechi hiyo pamoja na kuwa na mvuto, lakini haikuhudhuriwa na watu wengi kutokana na kufanyika katikati ya wiki.

    Leo Wambura ametuma taarifa kwamba, TFF na benki ya CRDB zimeunda kikosi kazi (task force) kwa ajili ya kushughulikia matumizi ya tiketi za elektroniki ambayo yalisimamishwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza.
    Taarifa ya Wambura imesema TFF na CRDB zimefanya kikao cha pamoja jana (Machi 20 mwaka huu) kuhusu masuala ya tiketi za elektroniki na kukubaliana kuunda kikosi kazi hicho kwa ajili ya uboreshaji matumizi ya mfumo huo.
    Amesema kikosi kazi hicho kitakuwa na wajumbe kutoka TFF na CRDB. Kwa upande wa TFF wajumbe wake ni Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama, Evodius Mtawala, yeye mwenyewe Wambura na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Silas Mwakibinga.
    Taarifa imesema Rais wa TFF, Jamal Malinzi ametoa shukrani za kipekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dr. Charles Kimei ambaye alihudhuria binafsi kwenye kikao akiongoza timu yake.
    Malinzi amesema ni imani ya TFF kuwa mfumo wa tiketi za elektroniki ndiyo mkombozi wa ulinzi wa mapato milangoni, na anaamini kwa pamoja TFF na CRDB zitafanikisha matumizi hayo ya tiketi za elektroniki.
    Wakati huo huo: Yanga inaumana na Rhino Rangers katika moja kati ya mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zitakazochezwa wikiendi hii katika miji miwili tofauti.
    Mechi hiyo itafanyika kesho (Machi 22 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora ambapo kiingilio kitakuwa sh. 5,000 kwa jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.
    Nayo JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika mechi itakayochezwa kesho Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Ligi hiyo itaendelea keshokutwa (Jumapili) kwa mechi nne ambapo Simba itacheza na Coastal Union katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam itaoneshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam Tv.
    Mechi nyingine za Jumapili ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAPATO YANGA NA AZAM YAIKWAMA TFF, YATANGAZA KUUNDA KIKOSI KAZI KUSHUGHULIKIA TIKETI ZA ELEKTRONIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top