• HABARI MPYA

    Friday, March 28, 2014

    SIMBA SC WAINGIA KAMBINI MABIBO KUIWEKEA AKILI SAWA AZAM

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    WAKATI uongozi ukishangazwa na matokeo mabovu ya timu yake licha ya wachezaji kulipwa mishahara na posho, kikosi cha mabingwa hapo wa zamani wa Tanzania Bara kinaingia kambini Mabibo jijini hapa kujiweka tayari kwa mechi ngumu dhidi ya vinara wa msimamo Azam FC Jumapili.
    Asha Muhaji, msemaji wa Simba SC, ameiambia BIN ZUBEIRY jijini hapa muda mfupi uliopita kuwa hakuna mchezaji ambaye hajalipwa mshahara lakini wanashangazwa na matokeo yasiyoridhisha ya kikosi chao kinachonolewa na Mcroatia Zdravko Logarusic.
    Mshambuliaji wa Simba SC, Zahor Pazi kulia. 

    Alisema kikosi chao kitaingia kambini kwenye hoteli kali maeneo ya Mabibo jijini hapa kukiwinda kikosi cha Mcameroon Joseph Omog cha Azam FC ambacho hakijapoteza hata mechi moja tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Agosti 24 mwaka jana.
    "Tunasikitishwa sana na matokeo ya timu yetu kwa sasa, tumepoteza mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union lakini hakuna mchezaji ambaye anadai mshahara au kutopewa posho. Tunalazimika kukubaliana na matokeo kwa sababu huu ni mpira na wakati mwingine unawakataa," amesema Asha.
    "Mechi ya Jumapili ni ngumu kutokana na ubora wa kikosi cha Azam lakini tutapambana kuhakikisha tunashinda walau mechi zote zilizobaki ili tumalize mahala pazuri ingawa ubingwa kwetu basi tena."
    Simba inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 36, 14 nyuma ya vinara Azam FC na 10 nyuma ya watani wao wa jadi Yanga ambao wanashikilia nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikikaliwa na Mbeya City.
    Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Simba SC iliyokuwa chini ya Abdallah 'King' Kibadeni, ililala 2-1 dhidi ya Azam FC iliyokuwa chini ya Muingereza Stewart John Hall.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAINGIA KAMBINI MABIBO KUIWEKEA AKILI SAWA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top