• HABARI MPYA

    Friday, March 21, 2014

    TFF YASITISHA MPANGO WA KUMTAMBULISHA MHOLANZI STARS

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    UTAMBULISHO wa kocha mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Martinus Ignatius ‘Mart’ Nooij sasa utasubiri hadi kuwasili kwa Mholanzi huyo mwishoni mwa mwezi huu, imefahamika.
    Awali, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ilikuwa afanye Mkutano na Waandishi wa Habari Machi 24 mwaka huu kumtaja rasmi mwalimu huyo, lakini sasa zoezi hilo litafanyika na Mholanzi huyo akiwa mezani.
    BIN ZUBEIRY inafahamu tayari Nooij ambaye kwa sasa ni kocha wa St George ya Ethiopia amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF na atakuja nchini mwishoni mwa mwezi huu.
    Kocha mpya Stars; TFF sasa itasubiri hadi Mart Nooij awasili nchini ndipo imtambulishe kuwa mwalimu mpya wa timu ya taifa

    Ulikuwa mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi ya soka ambao umefanikisha kupatikana mwalimu huyo wa Kiholanzi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
    Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
    Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
    Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12. 
    Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya  AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
    Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia anakoendelea na kazi hadi sasa.
    Baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili na TFF kuja kuifundisha Stars, Nooij anasubiri barua maalum ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kukamilisha taratibu za kuvunja Mkataba uliokuwa unaelekea ukingoni na klabu hiyo ya Addis Ababa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASITISHA MPANGO WA KUMTAMBULISHA MHOLANZI STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top