• HABARI MPYA

    Saturday, March 29, 2014

    MCHEZAJI WA AZAM FC 'KULA KISU' AFRIKA KUSINI

    BEKI wa pembeni wa Azam FC, Samih Hajji Nuhu atakwenda Afrika Kusini mwezi ujao kufanyiwa upasuaji wa goti, imeelezwa.
    Meneja wa Azam FC, Jemadari Said Kazumari ameiambia tovuti ya klabu kwamba, baada ya tiba za hapa nchini kushindwa kumrudisha uwanjani beki huyo Mzanzibari, sasa atapelekwa Afrika Kusini.
    Jemadari amesema kwamba, Daktari Mkuu wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa ndiye anayeshughulikia taratibu za Nuhu kwenda Afrika Kusini, ambako anatakiwa kufika kuanzia Aprili 10, mwaka huu.
    Kisu; Nuhu kushoto atafanyiwa upasuaji Afrika Kusini

    Nuhu amekuwa majeruhi tangu msimu uliopita baada ya kuumia goti na msimu wote huu amekuwa nje ya Uwanja.
    Mbali na beki huyo, wachezaji wengine majeruhi Azam FC ni beki wa kati, Ismail Gambo ‘Kussi Jr’ ambaye ataendelea kuwa nje kwa miezi miwili zaidi, viungo Joseph Kimwaga, Farid Mussa na Ibrahim Mwaipopo ambao wote watakuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja, maana yake kwa msimu huu hawatacheza tena.
    Kikosi cha Azam FC asubuhi hii kimeendelea na mazoezi yake Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, itakayopigwa Uwanja wa Taifa.
    Kikosi cha Joseph Marius Omog kinahitaji kushinda mchezo huo kesho ili kuendeleza kasi zake katika mbio za ubingwa dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC ambao nao kesho watacheza na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.  
    Azam FC ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 50 ilizovuna katika mechi 22 na imebakiza mechi nne, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 46 na imebakiza mechi tano.
    CHANZO:www.azamfc.co.tz
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHEZAJI WA AZAM FC 'KULA KISU' AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top