• HABARI MPYA

    Friday, March 21, 2014

    WABABE WA YANGA, AL AHLY WAENDELEZA REKODI MBAYA UGENINI, LEO WALALA TENA 1-0 TUNISIA

    Na Nurat Mahmoud, Tunis
    MABINGWA watetezi, Al-Ahly ya Misri wameendelea na rekodi yao mbaya ya mechi za ugenini baada ya jioni hii kufungwa bao 1-0 na Al Ahli Benghazi ya Libya katika mchezo wa kwanza wa Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika mchezo uliopigwa mjini Tunis, Tunisia. 
    Bao pekee lililoizamisha Ahly iliyoitoa Yanga SC ya Tanzania kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 1-1, jioni hii limefungwa na Mzimbabwe, Edward Sadomda dakika ya 67, akitumia vizuri makosa ya Nahodha ya mabingwa hao wa Afrika, Wael Gomaa.
    Wamepigwa tena; Al Ahly wamefungwa 1-0 mjini Tunis na Benghazi jioni ya leo 

    Hicho kilikuwa ni kipigo cha pili mfululizo cha ugenini kwa mabingwa hao mara nane barani, baada ya mwezi uliopita kufungwa na mabingwa wa Tanzania, Yanga SC mjini Dar es Salaam. 
    Timu ya Libya ilistahili ushindi leo na kuwapa faraja mashabiki wake waliosafiri hadi Tunis kutokana na mchezo mzuri uliofanyika katika Uwanja wao wa Benghazi.
    Washambulia Ahmed Zuway na Sadomba walilitia misukosuko mno lango la Ahly, lakini wakashindwa kufunga kwa bahati mbaya kipindi cha kwanza.
    Mara mbili, kipa wa Ahly, Sherif Ekramy aliinusuru timu yake kufungwa kwa kuokoa michomo ya Zuway aliyepiga kichwa dakika ya 23, kabla ya kuchupia mchomo wa Sadomba dakika saba kabla ya mapumziko.
    Ahli Benghazi ilitawala sehemu ya kiungo ikiongozwa na Nahodha, Abderahmane Fetori, aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Libya iliyotwaa Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Afrika Kusini Februari, mwaka huu akishirikiana vyema na Farag Mbarak, Solomon Jabason, Mosese Orkuma na Mmisri, Ahmed Eid.
    Dakika tano tangu kuanza kipindi cha pili, Mbarak alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kugonga mwamba pembeni.
    Baada ya kupelekwa mputa muda mrefu, kocha wa Ahly, Mohamed Youssef alimuingiza Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’ kuchukua nafasi ya Burkinabe Moussa Yedan dakika ya 66 kuimarisha timu yake, lakini walikuwa na Walibya waliopataa bao dakika moja baadaye.
    Mchezo wa marudiano utafanyika wiki ijayo na mshindi wa jumla atasonga mbele, wakati atakayetolewa ataingia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Mechi nyingine zitaendelea kesho TP Mazembe ya DRC ikiwa mgeni wa Sewe Sport mjini Abidjan, Horoya ya Guinea itaanzia nyumbani na CS Sfaxien ya Tunisia, sawa na ES Setif ya Algeria itakayoikaribisha Coton Sport ya Cameroon, AC Leopards ya Kongo itakayoikaribisha Al-Hilal ya Sudan na Nkana ya Zambia itakayoikaribisha Zamalek ya Misri, AS Vita ya DRC itaanzia nyumbani na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini Uwanja wa Tata Raphael mjini Kinshasa, wakati mechi zote za marudiano zitachezwa Jumamosi ya Machi 29, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WABABE WA YANGA, AL AHLY WAENDELEZA REKODI MBAYA UGENINI, LEO WALALA TENA 1-0 TUNISIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top