• HABARI MPYA

    Saturday, December 01, 2018

    YANGA YAMTEUA SAMUEL LUKUMAY KUCHUKUA NAFASI YA MANJI, KIKOSI CHAENDA MBEYA KWA NDEGE MECHI NA PRISONS JUMATATU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa klabu ya Yanga pamoja na kutaja majina saba ya watu wanaounda Kamati ya Uchaguzi, pia imemtambulisha Samuel Lukumay kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji.
    Hayo yanakuja siku chache baada ya uongozi wa Yanga kukutana na viongozi Kamati ya Utendaji na ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Uongozi huo ulitangaza majina hayo pamoja na kutaja rasmi Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo mara  baada ya vyombo vya usalama kusitisha mkutano wao wa dharula uliotakiwa kufanyika leo kwenye ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es Salaam.
    Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Siza Lyimo alimtangaza Samuel Lukumay kuwa kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo hadi pale uchaguzi utakapofanyika.

    Samuel Lukumay (kushoto) ameteuliwa kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga

    Pia Lyimo aliwataja wajumbe ambao wamewachagua kuingia kwenye kamati ya uchaguzi Yanga nao ni Jabir Katundu, Daniel Mlelwa, Samwel Mapande, Mustapha Nagar, Wakili Godfrey Mapunda, Edward Mwakingwe na Samwel Mangesho.
    Katika hatua nyingine, Lyimo alizungumzia kuhusu kusitishwa kwa mkutano wa klabu hiyo uliokuwa ufanyika leo, kuna baadhi ya wanachama wenzao walipeleka malalamiko kwa vyombo vya usalama ikiwemo Polisi kuwa mkutano huo ungekuwa na vurugu.
    Amesema amesikitishwa na kiongozi mmoja mkubwa ndani ya klabu hiyo kufuatia kuandika barua kwenda polisi na kuzuia  mkutano huo.
    "Nawaomba wanachama wa Yanga watulie, ipo siku tutatangaza tarehe nyingine ya mkutano,pale polisi watakapo jiridhisha mkutano kama utakuwa na amani,"alisema.
    Hata hivyo, Suzana alisema wapo baadhi ya viongozi wanapeleka maneno TFF na kusababisha Yanga kufuatiliwa kila mara.
    Aidha, viongozi  wa matawi wa klabu ya Yanga,wameendelea kushikiria msimamo wao wa kutohitaji kusimamiwa uchaguzi wao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na kusisitiza kuwa bado wanamtambua Yusuph Manji  kuwa ni Mwenyekiti wao.
    Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Makao Makuu ya klabu hiyo kwa niaba ya viongozi wenzake wa matawi, Mwenyekiti wa Kanda ya Kinondoni na Katibu wa tawi la Mazense, Shaaban Omary alisema kuwa wao hawapo tayari kufanya uchaguzi utakao simamiwa na TFF.
    Alisema kuwa kitendo cha TFF kuendelea kusimamia uchaguzi wa Januari 13, mwaka huu wao hawautambui na kueleza kuwa wanachama waliochukua fomu hawawatambui.
    "Uchaguzi unaosimamiwa na TFF sisi hatuutambui, sisi tunasubiria viongozi wetu watutangazie lini kutakuwa na uchaguzi  lakini huo mwingine hatuujui na hao waliochukua fomu hatuwatambui.
    Tunawaomba viongozi wa matawi wa wanachama wote waliochukua fomu TFF wawafute uwanachama kwani ni wasaliti," alisema.
    Wakati huo huo: Kikosi cha Yanga kimeondoka leo kwa ndege kuelekea mkoani Mbeya leo kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons Jumatatu.
    Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na watakuwa wanajifua kwa mara ya mwisho kabla ya mechi.
    Yanga kabla ya kuondoka iliifunga JKT kwa jumla ya mabao 3-0 na kujiweka kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 35.
    Katika nafasi ya pili wapo Azam walio na alama 33 huku Simba ikishika namba 3 ikiwa na alama 27.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAMTEUA SAMUEL LUKUMAY KUCHUKUA NAFASI YA MANJI, KIKOSI CHAENDA MBEYA KWA NDEGE MECHI NA PRISONS JUMATATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top