• HABARI MPYA

  Saturday, December 01, 2018

  KAMPUNI YA AFRIKA KUSINI YAMWAGA FEDHA KUDHAMINI LIGI KUU YA TANZANIA BARA, BODI YAPATA MWENYEKITI MPYA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kuwa shirikisho lipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu Tanzania bara na moja ya kampuni  ya Afrika Kusini, baada ya aliyekuwa mfadhili wa awali kampuni ya Vodacom kujitoa.
  Akizungumza leo kwenye mkutano wa tano wa Baraza Kuu la Bodi ya Ligi nchini (TPL), Karia alisema baada ya Vodacom kutaka kuwa mdhamini mdogo na kushindwa kufiakiana kwa baadhi ya vipengelee, na kuhangaika kutafuta mdhamini mwingine.
  Karia amesema shirikisho hilo linatambua mazingira magumu inayokumbana nazo klabu kwa kukosa udhamini, lakini mchakato wa kumpata mfadhili unaoendelea, utavisaidia hadi vilabu vya Ligi Daraja la Pili ikiwemo kuboresha zawadi kwa timu bingwa.
  “Kuna mwanga wa kupata mfadhili wa Ligi yetu, kuna kampuni moja ya Afrika Kusini inayouza bidhaa zake hapa nchini, tupo katika hatua za mwisho na ufadhili wao utasaidia vilabu vyetu na hata vile vya Ligi Daraja La Pili,” alisema Karia.
  Akizungumzia fedha za maendeleo ya soka zinazotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Karia alisema wapo katika hatua za mwisho za kurekebisha mapungufu yaliyosababisha shirikisho hilo kusitisha msaada kwa TFF tangu mwaka 2015.
  Alisema moja ya changamoto za kukosa fedha hizo ni namna ya matumizi mabaya ya fedha kwa uongozi uliopita lakini tayari FIFA wameridhishwa na uendeshaji wa TFF tangu walipoingia madarakani na kwamba fedha hizo sasa zitaanza kuletwa zote ambazo hazikuletwa.
  Karia alisema FIFA wataleta fedha zote kiasi cha dola za Kimarekani milioni 3 ambazo zinatokana na kiwango wanacholetewa kwa mwaka  dola 750,000 na kwamba sasa kwa utaratibu mpya fedha hizo zitakuwa dola milioni 1 kwa kila mwaka wataanza kuletewa.
  “Kiukweli FIFA waliiahidi serikali kwamba watazileta fedha hizo na tukifanikiwa kuzipata fedha hizo vilabu lazima navyo vipewe lakini vilabu vitakavyopata ni vile vitakavyokuwa na mfumo mzuri wa mahesabu ya fedha, Club Licensing (Leseni za vilabu) na timu za vijana,” alisema Karia.
  Karia alisema katika kuhakikisha vilabu vya Tanzania vinaendeshwa kisasa hivi karibuni wameingia mkataba wa mashirikiano na Ligi Kuu ya Hispania ‘Laliga’ ambapo kutakuwa na semina kwa viongozi wa vilabu kuhusu uendeshaji wa vilabu vyao semina zitakazofanyika mwezi ujao.
  Rais huyo wa TFF,Karia alisema kuanzia Januari mwakani anataka viwanja vyote vinavyochezwa Ligi Kuu waanze kutumia tiketi za Kieletroniki ili kuhikisha wanadhibiti mapato katika viwanja hivyo baada ya sasa viwanja viwanja vine tu vya Kaitaba mkoani Kagera, Taifa, Uhuru na Chamanzi vilivyopo Jijini Dar es salaam.
  Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga, Steven Mnguto amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) katika Uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Regal Naivera,Tanga.
  Nafasi zilizogombewa katika Uchaguzi huo mdogo ni Mwenyekiti,Mwakilishi wa Klabu za Daraja la Kwanza na Mwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili.
  Katika nafasi ya Mwenyekiti Steven Mnguto alikuwa Mgombea pekee aliyepigiwa Kura na Klabu za Ligi Kuu.
  Katika Kura 18 zilizopigwa Mnguto amepata Kura 16 za Ndio na Kura 2 za Hapana wakati Klabu 2 za Young Africans na African Lyon hazikuwa na muwakilishi.
  Kwenye nafasi ya Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Kwanza kulikuwa na Wagombea wawili Brown Ernest na Azim Khan Akbar,katika Kura 40 zilizopigwa Brown Ernest amepata Kura 18 na Azim Khan Akbar akipata Kura 22 hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Ally Mchungahela kumtangaza Khan kuwa ameshinda katika nafasi hiyo.
  Nafasi ya Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili ilikuwa na Mgombea mmoja Michael Kadebe katika Kura 40 zilizopigwa Kura 38 zilisema Ndio na Kura 2 zilisema Hapana hivyo Kutangazwa kuwa Muwakilishi wa Klabu za Daraja la Pili.
  Baada ya kutangazwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa TPLB,Steven Mnguto amewashukuru wapiga Kura wote walioshiriki kwenye Uchaguzi huo mdogo na ameahidi kuwa mtumishi mzuri kwa Klabu pamoja na kulinda maslahi ya Klabu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMPUNI YA AFRIKA KUSINI YAMWAGA FEDHA KUDHAMINI LIGI KUU YA TANZANIA BARA, BODI YAPATA MWENYEKITI MPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top