• HABARI MPYA

  Friday, November 02, 2018

  NAHODHA KELVIN YONDANI KUKOSEKANA YANGA MECHI DHIDI YA NDANDA FC JUMAPILI UWANJA WA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongo, Mwinyi Zahera atawakosa mabeki wake wawili Kelvin Yondani na Paul Godfrey ‘Boxer’ kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara watakapocheza na Ndanda FC.
  Yanga inatarajiwa kuvaana na Ndanda katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa saa kumi jioni huku wachezaji hao muhimu wakiukosa.
  Yondani ataukosa mchezo huo ni kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo uliopita huku Boxer akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata wakati timu hiyo ilipocheza na Lipuli FC ya Iringa.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari, Zahera alisema kukosekana kwa wachezaji hakumpi hofu kwani wapo wengine watakaocheza na kuziba nafasi zao vizuri, hivyo ana matarajio makubwa ya ushindi katika mchezo huo.
  Zahera alimtaja Vicent Andrew ‘Dante’ kuchukua nafasi ya Yondani ambaye amerejea uwanjani baada ya kupona majeraha yake ya misuli huku akimaliza adhabu ya kufungiwa mechi tatu za ligi na nafasi ya Boxer itachukuliwa na beki mkongwe, Juma Abdul.
  Kelvin Yondani atakosekana Yanga SC kwneye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC Jumapili

  Aliongeza kuwa, wakati wachezaji hao wakiukosa mchezo huo, anafurahia kurejea kwa kiungo wake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu ambaye ataiongoza Yanga katika mchezo huo na Ndanda.
  “Kukosekana kwa Yondani, Boxer kumesababisha nibadili mfumo wa uchezaji katika mchezo wangu na Ndanda niliokuwa nautumia katika michezo iliyopita kila mtu anafahamu kasi ya mabeki hao katia kupeleka mashambulizi.
   “Lakini licha ya Abdul kurejea katika timu hakumfanyi yeye kumuweka benchi au kumuondoa Boxer katika kikosi changu cha kwanza kwa sababu ya adhabu hiyo ya kadi aliyoipata, yeye Abdul hata acheze zaidi ya Cannavaro (Nadir Haroub) lakini hataweza kumtoa Boxer hilo analijua mwenyewe,” alisema Zahera na kuongeza kuwa.
  “Timu yangu imejiandaa vema kuhakikisha inaendeleza rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo wa ligi katika uwanja wetu wa nyumbani kabla ya kutoka katika mcheo ujao wa ligi.
  “Kabla ya ligi kuanza tukiwa kambini Morogoro niliwaambia wachezaji wangu hatutakiwi kupoteza mchezo katika uwanja wetu ni lazima tushinde ili tujiwekee mazingira mazuri ya ubingwa,”alisema Zahera.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NAHODHA KELVIN YONDANI KUKOSEKANA YANGA MECHI DHIDI YA NDANDA FC JUMAPILI UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top