• HABARI MPYA

  Sunday, November 11, 2018

  KAPTENI MKUCHIKA ATANGAZA RASMI MANJI KUREJEA MADARAKANI YANGA SC, ASEMA ATAINGIA OFISNI JANUARI 15

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BARAZA la Wadhamini la klabu ya Yanga SC leo limethibitisha kurejea kwa Yussuf Manji kuendelea kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.
  Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Kapteni Mstaafu, George Huruma Mkuchika alipozungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam leo.
  Mkuchika amesema kwamba kufuatia tamko la kurejea kwa Manji, nafasi ya Uenyekiti haitajazwa katika uchaguzi ujao Januari 13, mwakani.
  Mkuchika aliionyesha na kuwasomea Waandishi wa Habari barua iliyoandikwa na Manji kujibu ombi la wanachama wa klabu hiyo kumtaka aendelee na nafasi hiyo kufuatia yeye kuandika barua ya kujiuzulu Mei mwaka jana baada ya miaka 11 akianza kama mfadhili mwaka 2006.


  Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Kapteni George Mkuchika (kulia) akiwa na Mjumbe wa Baraza hilo, Dk. Jabir Katundu wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari

  Wanachama wa Yanga walikataa ombi la Manji kujiuzulu katika mkutano wa Juni 10, mwaka huu Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay mjini Dar es Salaam.
  “Kifupi anasema, nimepokea uamuzi wa wanachama wa Yanga, kwa bahati mbaya kipindi ninachoandikiwa mimi nipo kwenye matibabu, tarehe 15 Desemba madaktari wangu wanasema nitakuwa nimekamilika. Kwa hiyo pamoja na kwamba nimerudi kama Mwenyekiti, nitafanya kazi za kwenda ofisini kila mara kuanzia tarehe 15 Januari,”amesema Mkuchika akiisoma barua hiyo. 
  Mkuchika amesema Januari 15 Manji ataanza rasmi kazi za Yanga na kwenye makampuni yake baada ya kupitia kipindi kirefu cha misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka jana, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye kuwekwa rumande akidaiwa kumiliki pasipoti mbili na uhujumu uchumi, kesi ambazo zote zilifutwa.
  Katika hatua nyingine, Mkuchika amepinga uchaguzi wa klabu hiyo kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  “Suala lingine ambalo limeleta sitofahamu, ni uchaguzi wa Yanga kusimamiwa na TFF, kila klabu iliyosajiliwa kwa Msajili ina taratibu zake za kuwachagua viongozi wake, sijui kama itaanza Yanga mara ya kwanza,”.
  “Tumewaita viongozi wa kamati ya Utendaji wametuambia Kamati ya uchaguzi wanayo, ipo hai, lakini sisi Baraza la wadhamini tukasema, hata kama Kamati ya Uchaguzi ya Yanga haipo, wanatakiwa waunde Kamati ya uchaguzi ili isimamie uchaguzi. Uchaguzi wa Yanga kusimamiwa na Kamati ya uchaguzi isiyo ya Yanga tunavunja katiba ya Yanga,” alisema Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 
  Uchaguzi mdogo wa Yanga SC kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu baadaa ya kuchaguliwa Juni mwaka 2016 unatarajiwa kufanyika Januari 13 mwakani na baada ya kurejea kwa Manji, nafasi zitakazojazwa ni Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah waliojiuzulu.  
  Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Manji ni Wajumbe wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
  Fomu za wagombea zinatolewa makao makuu ya klabu Sh. 200,000 kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Sh. 100,000 kwa Ujumbe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAPTENI MKUCHIKA ATANGAZA RASMI MANJI KUREJEA MADARAKANI YANGA SC, ASEMA ATAINGIA OFISNI JANUARI 15 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top