• HABARI MPYA

  Saturday, November 03, 2018

  KAGERE APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAICHAPA JKT 2-0 MKWAKWANI, MTIBWA SUGAR YAITANDIKA 4-0 RUVU SHOOTING

  Na Nasra Omary, TANGA
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamerejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Shujaa wa Wekundu wa Msimbazi leo ni mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha kwanza.
  Kwa ushindi huo, Simba SC ya kocha Mbelgiji Patrick J. Aussems inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 11, ikirejea nafasi ya pili, nyuma ya Azam FC yenye pointi 27 za mechi 11 na mbele ya Yanga SC, yenye pointi 25 za mechi tisa.

  Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza Msimbazi, yalipo makao makao makuu ya Simba SC aliwafungia bao la kwanza Wekundu hao dakika ya 11 akimalizia pais ya mshambuliaji mwenzake, Mganda Emmanuel Arnold Okwi.
  Na Kagere akafunga tena dakika ya 37 akimalizia mpira uliogonga mwamba baada ya kumchanganya kipa wa JKT Tanzania, Abdalrahiman Mohamed ‘Wawesha’ kufuatia shuti la mpira wa adhabu la Okwi. 
  Kipindi cha pili, JKT Tanzania inayofundishwa na kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ ilibadilika na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba kusaka mabao.
  Lakini bahati haikuwa yao, kwani pamoja na kushindwa kupata bao walimpoteza mchezaji wao mmoja, Ally Ahmed ‘Shiboli’ aliyetolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 88 baada ya kumfanyia fujo refa akilalamikia kunyimwa penalti kutokana na beki wa Simba SC, Erasto Nyoni kuunawa mpira kwenye boksi.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Martin Kiggi dakika ya 90 na ushei limeipa ushindi wa 1-0 Alliance FC dhidi ya Singida United Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Nayo Mtibwa Sugar imeipapasa Ruvu Shooting kwa kuichapa 4-0, mabao ya Kelvin Sabato dakika ya 53, Salum Kihimbwa dakika ya 56, Juma Luizio dakika ya 63 na Jaffar Kibaya dakika ya 90 na ushei, wakati Biashara United imelazimishwa sare ya 0-0 na Mbao FC Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.    
  Kikosi cha JKT Tanzania kilikuwa; Abdalrahiman Mohamed ‘Wawesha’, Anuary Kilemile, Sajkim Gilla, Frank Nchimbi, Rahim Juma, Madenge Ramadhan, Mwinyi Kazimoto, Kelvin Nashon/Nassoro Kapama dk67, Hasan Materema, Abdalahman Mussa/Ally Ahmed dk57 na Edward Songo.
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Hassan Dilunga/Shizza Kichuya dk70, Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERE APIGA ZOTE MBILI SIMBA SC YAICHAPA JKT 2-0 MKWAKWANI, MTIBWA SUGAR YAITANDIKA 4-0 RUVU SHOOTING Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top