• HABARI MPYA

    Thursday, November 09, 2017

    YANGA YAADHIBIWA KWA MASHABIKI WAKE KUMWAGA MIKOJO UWANJANI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wametozwa faini ya Sh. 500,000 baada ya mashabiki wake kutuhumiwa kurusha uwanjani chupa zilizokuwa na mikojo wakati wa mchezo dhidi ya mahasimu wao, Simba.
    Adhabu hiyo imetolewa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kupitia ripoti za michezo yote ya Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja Pili.
    Katika mechi hiyo namba 58 iliyomalizika kwa sare ya 1-1, bao la Somba likifungwa na Shiza Kichuya na la Yanga likifungwa na Mambia, Obrey Chirwa, adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Nao mahasimu wao, Simba wamepewa onyo Kali kutokana na Kocha wake Msaidizi, Mrundi Masoud Juma kuanza kufundisha bila kuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini. 
    Katika mechi hiyo namba 54, Simba ilishinda 4-0 na uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 40(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
    Klabu hiyo pia imetakiwa kufikia Novemba 10 iwe imewasilisha Bodi ya Ligi nakala ya vibali hivyo, na kukumbushwa kuwa mahitaji ya nyaraka hizo ni kwa mujibu wa Kanuni za Ligi, lakini pia sheria za nchi.
    Vilevile klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa timu yake kuwasilisha orodha ya wachezaji wake (team match list) nje ya muda wa kikanuni. Kitendo cha timu hiyo ni kukiuka Kanuni ya 14(2k) ya Ligi Kuu. Adhabu dhidi yao imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
    Klabu ya Njombe Mji imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonesha vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina katika mechi hiyo wakati ikiwasili uwanjani. Adhabu dhidi ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.
    Mechi namba 56 (Stand United 0 v Yanga 4). Klabu ya Stand United imetozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kutokana na golikipa wao kuvaa jezi yenye namba tofauti na ile iliyosajiliwa, kitendo ambacho ni ukiukaji wa Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu kuhusu Usajili. Adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 60(12) ya Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAADHIBIWA KWA MASHABIKI WAKE KUMWAGA MIKOJO UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top