• HABARI MPYA

  Friday, March 10, 2017

  TFF YAZITILIA UBANI YANGA NA AZAM MICHUANO YA AFRIKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limezitakia la kheri timu za Yanga na Azam FC katika mechi zao za michuano ya Afrika wikiendi hii.
  Yanga watamenyana na Zanaco ya Zambia kesho katika mechi ya kwanza ya hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC watakuwa wenyeji wa Mbabane Swallows ya Swaziland katika mechi ya kwanza hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
  Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema leo kwamba maandalizi ya mechi zote mbili yamekamilika na mchezo wa kesho utaanza Saa 10.00 jioni ukichezeshwa na maarefa kutoka Djibouti, Djamal Aden Abdi atakayesaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime, wakati refa wa akiba atakuwa Souleiman Djamal na Kamisaa Luleseged Asfaw kutoka Ethiopia.
  Viingilio vya kesho ni Sh 20,000 kwa VIP ‘A’, Sh 10,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ na Mzunguko (Viti vya Rangi ya chungwa, kijani na bluu) ni Sh 3,000.
  Mechi ya Azam na Mbabane Swallows ya Swaziland Jumapili Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam, itachezeshwa na marefa kutoka Benin, Addissa Abdul Ligali na wasaidizi ni Medegnonwa Romains Agbodjogbe na Babadjide Bienvenu Dina huku Mwamuzi wa akiba akiwa Moumouni Kiagou na kamisha wa mchezo atakuwa Mohamed Omar Yusud wa Kenya.
  Viingilio katika mchezo huo ni Sh 10,000 kwa VIP, Jukwaa Kuu itakuwa ni Sh 5,000 na Mzunguko itakuwa ni Sh 3,000.
  Wakati huohuo, tiketi za waamuzi wa Tanzania walioteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu za AS Porto Louis 2000 ya Mauritius na El Hilal ya Sudan wikiendi ijayo, wamepata tiketi zao za kusafiri.
  Katika mchezo huo ambao utafanyika ama Machi 17, 18 au 19 Mwamuzi wa kati atakuwa Israel Mujuni Nkongo wakati wasaidizi wake watakuwa ni Samuel Hudson Mpenzu na Josephat Deu Bulali huku Mwamuzi wa akiba akiwa ni Hery Sasii. Kamisha katika mchezo huo Na. 78 atakuwa Jerome Kelvyn Damon kutoka Afrika Kusini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAZITILIA UBANI YANGA NA AZAM MICHUANO YA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top