• HABARI MPYA

    Monday, November 21, 2016

    YANGA YATAMBULISHA BENCHI JIPYA LA UFUNDI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE klabu ya Yanga leo imemtambulisha rasmi, Mzambia George Lwandamina kuwa kocha wake mpya na Hans van der Pluijm kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga amesema Lwandamina ataanza kazi rasmi mwishoni mwa mwezi. 
    "Ni kweli tumeingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United nchini Zambia. Lwandamina ataanza kuifundisha timu yetu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu"
    George Lwandamina anakuwa kocha mpya Yanga SC na Hans van der Pluijm atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi

    Aidha, Sanga amesema kocha wao wa sasa, Pluijm ataendelea na kazi, isipokuwa anahamia kwenye Ukurugenzi wa Ufundi. "Ni mwalimu mzoefu na anaijua vyema Yanga SC, hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kwa ujumla,"alisema Sanga na kuongeza.
    "Mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha Pluijm kilikuwa kibaya, bali uongozi katika hatua ya kuiboresha klabu yake umeamua kuleta changamoto mpya ili kujiweka bora zaidi katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo,". 
    Sanga amesema Lwandamina atjiunga na timu mara wachezaji watakaporejea kutoka mapumzikoni na kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    "Likizo waliyopewa inakwisha tarehe 25 na uongozi unatarajiwa kuweka kambi nje ya nchi kwa maandalizi yakinifu ya mzunguko wa pili wa ligi kuu unaoanza rasmi Desemba 17,"amesema Sanga. 
    Pamoja na hayo, Sanga amesema Juma Mwambusi ataendelea kuwa Kocha Msaidizi wa klabu hiyo hadi hapo itakapotangazwa tofauti. 
    "Mara nyingi kocha mkuu ndiye anaamua au kupendekeza msaidizi wake na sio klabu, hivyo bado Mwambusi ni kocha wetu hadi hapo itakapotangazwa tofauti. Klabu kwa sasa imejikita kwa hao wawili wakubwa wa juu,"alisema.
    Chini ya Pluijm na Mwambusi, Yanga ilimaliza nafasi ya pili katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa pointi zake 33, ikizidiwa mbili na vinara, Simba SC waliomaliza na pointi 35. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YATAMBULISHA BENCHI JIPYA LA UFUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top