• HABARI MPYA

    Tuesday, November 22, 2016

    MAKOCHA WA AZAM NA YANGA WAFUNGIWA NA TFF KWA UBABE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAKOCHA Wazungu, Zeben Hernandez Rodriguez wa Azam FC kutoka Hispania na Hans van Pluijm wa Yanga kutoka Uholanzi wamefungiwa mechi tatu kila mmoja mara tu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakapoanza mwakani.  
    Taarifa ya Kamati ya Saa 72 ya Uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyotolewa leo, imesema kwamba Pluijm ameadhibiwa kutokana na makosa aliyoyafanya katika mechi namba 59 kati ya Yanga na Ruvu Shooting.
    Pluijm amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu baada ya wakati wa mapumziko kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. Pia baada ya mechi kumalizika alikwenda kwenye chumba cha waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa. 
    Mholanzi Hans van Pluijm wa Yanga amefungiwa mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 

    Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 40(1).Ruvu Shooting imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 12, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.
    Yanga nayo imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kuwazonga waamuzi na kuwatolea maneno ya kashfa walipokuwa wakiingia vyumbani wakati wa mapumziko. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).
    Mechi namba 116 (Mbao FC Vs Azam FC). Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi (ordered off) kwa kukataa kuheshimu mipaka ya eneo la ufundi (technical area) katika mechi hiyo. Adhabu imezingatia Kanuni ya 40(11).
    Mchezo namba 90 (Simba Vs Toto Africans). Klabu ya Toto Africans imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanja kwa dakika saba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu. 
    Mechi namba 99 (Mwadui Vs Simba). Klabu zote mbili zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango wa washabiki, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48). 
    Mechi namba 101 (Ruvu Shooting Vs Stand Utd). Ndanda FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi,  kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48). 
    Nayo Ruvu Shooting ambayo ilikuwa uwanja wa nyumbani, imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 15. Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu, na adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48). 
    Mechi namba 104 (JKT Ruvu Vs Ndanda). Klabu ya Stand United imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake kufanya vurugu wakitaka kuingia uwanjani bila ya kuwa na uthibitisho kuwa wao ni wachezaji wa timu hiyo wakati wa mechi kati ya JKT Ruvu na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 42(1). 
    Mechi namba 112 (Majimaji Vs JKT Ruvu). Daktari wa JKT Ruvu, Abdullah Yusuf amefungiwa miezi mitatu, na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kusababisha usumbufu kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, na kuwatolea maneno machafu Mwamuzi na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 41(2). 
    Mtaalamu wa viungo wa JKT Ruvu, George Minja amefungiwa miezi mitano na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumvamia Mwamuzi akitaka kumpiga, na pia kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi baada ya mechi hiyo. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2). 
    Nao wachezaji wa JKT Ruvu, Said Kipao jezi namba moja, Samwel Kamuntu (22), Pela Mavuo (16) na paul Mhidzhe (23) wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwatukana waamuzi baada ya mchezo kumalizika. Adhabu imezingatia Kanuni ya 37(7). 
    Mechi namba 117 (Ndanda Vs Stand Utd). Katika mechi hiyo kadri muda ulivyokuwa ukienda ball boyz walichelewesha kurudisha mipira uwanjani, na mbaya zaidi mipira ilikuwa ikifichwa kiasi cha kubaki miwili kati ya sita iliyokuwepo. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ili ahakikishe suala hilo halijitokezi tena.
    Mechi namba 60 (Tanzania Prisons Vs Simba). Klabu ya Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) na kufika wakati taratibu zote za msingi zikiwa zimemalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu.
    Klabu zote (Tanzania Prisons na Simba) zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kuingia uwanjani kwa milango isiyo rasmi. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 14(14), na adhabu imezingatia Kanuni ya 14(48).
    Prisons pia imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya gari la Jeshi la Magereza namba MT 0084 aina ya Toyota Land Cruiser Pick Up likiwa na watu 15 kuingia uwanjani kwa nguvu, na kusababisha kupigwa na kuumizwa kwa mlinzi wa getini. Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1).
    Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kutoka Morogoro amepewa onyo kali kwa kutoripoti baadhi ya matukio ya wazi yaliyotokea kabla ya mechi hiyo kuanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAKOCHA WA AZAM NA YANGA WAFUNGIWA NA TFF KWA UBABE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top