• HABARI MPYA

    Tuesday, November 22, 2016

    MAKONDA AWASHUKURU, AWAPONGEZA AZAM

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda, leo mchana amefanya ziara kwenye Makao Makuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC akiwa na lengo kuu la kuipongeza kutokana na juhudi kubwa wanazofanya za kuwekeza katika soka la Tanzania.
    Mbali na kuipongeza Azam FC inayomilikiwa na familia ya mmoja ya wafanyabiashara maarufu Afrika, Alhaji Said Salim Bakhresa, pia ametoa shukrani zake kutokana na jitihada zinazoonyeshwa na mfanyabiashara huyo mzawa katika maeneo mengine aliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye tasnia ya habari (Azam Media) na viwanda.
    Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi (kushoto akimkabidihi jezi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo

    Kwenye msafara huo, Makonda aliambatana baadhi ya viongozi wengine wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, alikofanya ziara tofauti kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Jackson Lyanivana.
    Ugeni huo ulipokelewa na viongozi wa juu wa Azam FC, wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa, Meneja wa timu, Phillip Alando, ambao katika kumalizia ziara hiyo waliweza kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali yaliyofanyiwa uwekezaji ndani ya Azam Complex.
    Akitoa neno lake kwenye ziara hiyo, Makonda alisema haina ubishi kuwa Azam FC ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwekeza ipasavyo kwenye soka huku akidai kuwa timu hiyo imeshaanza kwa vitendo kutekeleza suala la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini.
    “Leo hii mnatuunga mkono zaidi kwa sababu ni kiwanja kimoja na ni timu moja ambayo kila mtu aliyeko Dar es Salaam anaizungumzia, katika suala zima la kupunguza idadi ya vijana walioko mtaani wasiokuwa na dira wala matumaini nyinyi Azam mmeshaanza kutekeleza kwa vitendo na watu wote hatuwezi kuajiriwa serikalini, haiwezekani leo serikali ikaajiri watu wote.
    “Inawezekana kabisa kila mtu na kipaji chake anaweza akafanya vizuri na mwisho wa siku akaendesha maisha yake, kwa hiyo tunawashukuru sana sana sana Azam FC,” alisema.
    Makonda alichukua fursa hiyo pia kutoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitokeza, na kuiga mfano wa watu wa Azam FC ili kuwa na timu nyingi zenye ushindani na kuondoa migogoro kwenye soka la Tanzania.
    “Waige mfano wa Azam, watengeneze timu zao, watengeneze viwanja ili tuwe na watu wengi, tuwe na timu nyingi zenye ushindani na hata hii migogoro migogoro inayotokea Yanga na Simba, wenye hela zao wasihangaike, kama wamegoma kukodishwa waje tu watengeneze timu zao ili na wenyewe waendelee kunufaika kwa sababu mwisho wa siku tunajua tukiwa na timu nyingi kama ilivyo Azam FC, ikapatikana timu nyingine ya watu wenye uwezo kama nyie mnavyowajali vijana wenu ushindani utakuwa mkubwa sana.
    “Na hivyo ndivyo tunaweza kuweka vijana wengi wakawa kwenye vipaji vyao tukajenga uchumi wetu kupitia ajira inayotokana na michezo na mwisho wa siku tukapeperusha vema bendera ya Taifa letu katika mataifa mbalimbali katika sekta nzima ya michezo, mimi naamini kwa kazi na mfano mnaoonyesha niwaombe watu wengine waendelee kuiga,” alisema.
    Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Makonda amewaomba Watanzania waendelee kununua bidhaa zinazotengenezwa na wazawa akitolea mfano baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na makampuni ya Bakhresa.
    “Mfano kama hivi viwanda vyenu vinatengeneza juisi, mnatengeneza maji, mnatengeneza ngano, walioajiriwa ni Watanzania wenzetu kwa hiyo kadiri mnavyouza bidhaa zenu manake kuna uhakika wa kupanua biashara, mkipanua biashara wadogo zetu, kaka zetu wanapata ajira lakini la pili mkiendelea kuuza mnalipa kodi, ile kodi tunapata barabara, madawa, tunapata shule, tunapata kila kitu tunachokitafuta,” alisema.
    Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, alimshukuru Makonda kwa ugeni wake huo ndani ya klabu hiyo, huku akichukua fursa hiyo pia kumwelezea historia fupi ya Azam tokea ianzishwe mwaka 2004 hadi ilipo mpaka sasa.
    Mbali na historia, alimweleza timu mbalimbali zilizoko ndani ya Azam Complex, timu ya vijana (U-20) na ile ya wakubwa pamoja na mipango kabambe inayoendelea ya kuunda timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15 na 17, mchakato unaoelekea ukingoni ukihusisha mikoa mbalimbali.
    “Baada ya michuano ya Copa Coca Cola kutokuwa na mwelekeo, kama klabu tumeamua kuwafuata vijana kule walipo tumefanya majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam, tumekwenda Zanzibar, Tanga, Morogoro na wiki iliyopita tulikuwa mkoani Mbeya tulikopata vijana saba, bado tutaendelea kufanya uwekezaji tutaenda mkoani Tabora, Mwanza, Kigoma na Mtwara,” alisema.
    Aliongeza kuwa: “Kwa hiyo sisi tunaamini ya kuwa hata Mheshimiwa hapa Mkuu wa Mkoa utakuwa ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa wa kutusapoti na karibu sana Azam FC usichoke kuja wakati wowote…Yote tunayoyafanya ni kutokana na kampuni mama ya Azam na wadhamini wetu ambao ni Benki ya NMB lakini haitoshi kwa hiyo tunachukua fursa hii kuyaomba makampuni mengine ambayo yanaweza kuona nafasi ya wao kuwekeza waje, tuna timu za vijana, njooni mfanye kazi na sisi tuweze kusomba mbele.”
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAKONDA AWASHUKURU, AWAPONGEZA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top