• HABARI MPYA

    Wednesday, November 30, 2016

    YANGA WAWAKIMBIA SIMBA POLISI, KESHO MAZOEZI GYMKHANA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC wameamua kuhama Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam ili kuwakwepa mahasimu wao, Simba.
    Yanga walianza mazoezi juzi Uwanja wa Polisi Kurasini kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, lakini jana jioni mahasimu wao, SImba walikutana hapo pia kwa mkakati wa kuanza mazoezi leo.
    Kukwepa kufanya mazoezi Uwanja mmoja na mahasimu wao, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema leo akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online kwamba kesho wanahamia kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.
    “Simba wao wamekuwa wakitufuata fuata kila sehemu tunayokwenda, tulianza kule Boko Veterani, wakatufuata. Hata huku Polisi tulianza sisi, wakatufuata pia, sasa tunakwenda Gymkhana tuone kama nako wana jeuri ya kutufuata,”amesema Hafidh.
    Yanga wamehama Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Polisi, Kurasini, Dar es Salaam ili kuwakwepa mahasimu wao, Simba 

    Pamoja na hayo, Hafidh amesema kwamba wachezaji watatu waliongezeka mazoezini jana asubuhi Polisi Kurasini ambao ni kipa Benno Kakolanya, beki Hassan Kessy na kiungo Haruna Niyonzima.
    Watatu hao wanafanya idadi ya wachezaji 21 kuhudhuria mazoezini Yanga ndani ya siku mbili, baada ya 18 waliojitokeza katika siku ya kwanza.
    Waliofika mapema Jumatatu ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Wengine ni viungo Simon Msuva, Deus Kaseke, Mkongo Mbuyu Twite, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Matheo Anthony.
    Kinda Yussuf Mhilu aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana, yupo na kikosi cha U-20 Bukoba mkoani Kagera kwenye Ligi Kuu ya Vijana.
    Ambao bao hawakufika mazoezini ni beki Mtogo Vincent Bossou, washambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, Mzambia, Obrey Chirwa na wazawa kiungo Yussuf Mhilu na mshambuliaji Malimi Busungu.
    Lakini Hafidh amesema Ngoma aliwasili jana jioni, hivyo leo ataungana na wenzake, wakati Chirwa alitarajiwa kuwasili kuanzia jana. “Busungu pia tunamtarajia leo, Bossou ana ruhusa maalum, Mhilu yupo na kikosi chetu cha U-20 kwenye Ligi Kuu ya Vijana,”amesema Hafidh.
    Yanga ilianza mazoezi jana Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam chini ya benchi la jipya lam Ufundi, lililopanuliwa kufuatia ujio wa kocha mpya, Mzambia, Geeorge Lwandamina anayechukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm anayehamia kwenye Ukurugenzi wa Ufundi.
    Na Yanga inajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAWAKIMBIA SIMBA POLISI, KESHO MAZOEZI GYMKHANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top