• HABARI MPYA

    Friday, November 25, 2016

    LWANDAMINA: SITABADILI CHOCHOTE KWENYE BENCHI LA UFUNDI YANGA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu mpya wa Yanga SC, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba atafanya kazi na Maofisa aliowakuta benchi la Ufundi na hataleta mtu mpya.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam wakati wa utambulisho wa wakuu wapya wa Idara ya Ufundi, Lwandamina alisema kwamba hana mpango wa kubadilisha chochote kwenye benchi la Ufundi.
    Na kuhusu kuongeza wachezaji, Lwandamina amesema kwamba ameiona Yanga katika mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikishinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting na amegundua ni timu nzuri ambayo haihitaji mchezaji mpya.
    Lwandamina (kulia) amesema hatabadilisha chochote kwenye benchi la Ufundi. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga

    Alimsifu mtangulizi wake, Pluijm kwamba amefanya kazi nzuri na akasema atafuata nyayo zake na atashirikiana naye bega kwa bega kuhakikisha Yanga inapata mafanikio zaidi.
    Lwandamina amekana madai kwamba amependekeza wachezaji wawili aliokuwa nao Zesco United ya kwao, Zambia kiungo Misheck Chaila na mshambuliaji Mkenya Jesse Were wasajiliwe pia. 
    Baada ya kuiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128 kwenye awamu mbili, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23, Pluijm aliyetua Jangwani mwaka 2014 anampisha Lwandamina.
    Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
    Na anahama nafasi baada ya msimu mzuri uliopita, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
    Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita. 
    Benchi jipya la Ufundi Yanga sasa linakuwa chini ya Pluijm kama Mkurugenzi, Lwandamina Kocha Mkuu, Juma Mwambusi Kocha Msaidizi, Juma Pondamali Kocha wa makipa, Hafidh Saleh Meneja, Daktari Edward Bavu, Jacob Onyango Mchua Misiliu na Mtunza Vifaa Mohamed Omar ‘Mpogolo’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA: SITABADILI CHOCHOTE KWENYE BENCHI LA UFUNDI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top