• HABARI MPYA

    Tuesday, November 22, 2016

    TFF YAMFUNGIA ULIMWENGU WA POLISI MIEZI SITA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Saa 72 ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia kiongozi wa Polisi Dar es Saaam, Ulimwengu Hamimu miezi sita kutojihusisha masuala ya soka. 
    Ulimwengu ambaye hana uhusiano wowote na mshambuliaji wa zamani wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu, anakutana na adhabu hiyo pamoja na faini ya Sh. 200,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 41(2), baada ya makosa aliyoyafanya katika mechi namba 17 kati ya Polisi Dar na Ashanti Utd. 
    Ulimwengu alichukua mpira na kuupiga kwenye jukwaa la timu ya Ashanti Utd na kutaka kumpiga Mwamuzi akiwa na mchezaji wake Pascal Theodory mwenye jezi namba 15.
    Mchezaji huyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 100,000. 
    Mechi namba 19 (Pamba Vs African Sports). Klabu ya African Sports imepewa onyo kali kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) kwa dakika nne, na kufika na viongozi watatu badala ya wanne. 
    Mchezaji Shaaban Kimaro amefungiwa mechi sita na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kumpiga kichwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili. Mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa hilo alilolifanya dakika 83. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi daraja la Kwanza.
    Naye Salum Omari pia wa African Sports amefungiwa mechi tatu na faini sh. 300,000. Akiwa mchezaji wa akiba aliingia uwanjani kwa nia ya kutaka kumshambulia Mwamuzi, lakini Polisi walimuwahi na kumtoa. 
    Mechi namba 20 (Kiluvya Utd Vs Mshikamano). Mchezaji Ayoub Upatu wa Mshikamano amesimamishwa na suala lake limepelekwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kwa hatua zaidi baada ya Kiluvya Utd kuwasilisha pingamizi dhidi yake kuwa ni mchezaji wao, kwani wana leseni yake. Katika leseni ya Kiluvya Utd ametumia jina la Ayoub Kassim Lipati. 
    Mechi namba 25 (Ashanti Utd Vs Lipuli). Kamati imetupa malalamiko ya timu ya Lipuli dhidi ya Ashanti Utd kuwa katika mechi yao ilimchezesha mchezaji Patrick James mwenye jezi namba 15 wakati akiwa na kadi tatu za njano. Kamati imebaini wakati James akicheza mechi hiyo alikuwa na kadi mbili za njano, na si tatu. 
    Mechi namba 27 (Kiluvya Utd Vs Friends Rangers). Kocha Msaidizi wa Friends Rangers, Fadhili Ndumba amefungiwa mechi mbili na faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi na Mwamuzi kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi Msaidizi Namba Moja. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
    Mechi namba 23 (Kurugenzi Vs Kimondo). Viongozi wa Kimondo, Eric Ambakisye, Selestine Mashenzi, na Mussa Minga wamefungiwa miezi sita, na kupigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kuwafuata waamuzi hotelini baada ya mechi ambapo walimpiga Mwamuzi Mussa Gabriel na kumjeruhi wakishirikiana na baadhi ya wachezaji wao. 
    Wachezaji waliohusika katika tukio hilo ambapo wamefungiwa mechi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja ni; January Daraja Mwamlima, Daniel Douglas Silvalwe, Abiud Kizengo na Monte Stefano Mwanamtwa. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 24(6) ya Ligi Daraja la Kwanza. 
    Mechi namba  23 (Alliance Vs Mvuvumwa). Kocha Msaidizi wa Mvuvumwa, Ezekiel Chobanga amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi dakika ya 59 kwa kumtolea lugha chafu Mwamuzi. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza. 
    Mechi namba 24 (Polisi Dodoma Vs Rhino Rangers). Mchezaji Sameer Mwishehe wa Rhino Rangers amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumrushia Mwamuzi chupa ya maji baada ya mchezo kumalizika. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza. 
    Mechi namba 25 (Polisi Dodoma Vs Mgambo Shooting). Kocha wa Mgambo, Athuman Kairo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumshambulia kwa maneno Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 40(11). 
    Mechi namba 28 (Alliance Vs Singida Utd). Baada ya Alliance kupata bao, watu wa huduma ya kwanza walipokuwa wakiitwa kuingia uwanjani, walikuwa wanakwenda kwa kupoteza muda. Msimamizi wa Kituo ameandikiwa barua ya kuwakumbusha watu wa huduma ya kwanza kutekeleza majukumu yao wawapo uwanjani, na kuhakikisha kuwa tukio la aina hiyo halitokei tena.
    Aidha, Kamati imeridhia maombi ya timu ya Mvuvumwa kuhamishia mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kutoka Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma. Hivyo, kuanzia Mzunguko wa Pili wa SDL, mechi za Mvuvumwa zitachezwa mjini Shinyanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAMFUNGIA ULIMWENGU WA POLISI MIEZI SITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top