• HABARI MPYA

    Sunday, November 27, 2016

    YANGA IKIMTUMIA KWA FAIDA PLUIJM ITATAMANI KUWA NAYE DAIMA MILELE

    NI vigumu kwa namna yoyote jina la Tambwe Leya (sasa marehemu) kukosekana kwenye historia ya klabu ya Yanga.
    Yanga ilimpata kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mwaka 1974 ilipokwenda Brazil kwa ziara ya mafunzo.
    Ilimkuta akiwa anasomea ukocha nchini humo na ili kukwepa gharama za kummiliki kocha wake wa wakati huo, Profesa Victor Stanslescu, aliyefanya kazi ya kihistoria Jangwani, iliamua kumchukua Mkongo huyo.
    Mshahara aliokuwa akilipwa Tambwe haukufika hata nusu ya mshahara wa kocha Mromania, Dk Victor. Victor naye ni kocha wa kihistoria pia Jangwani, alianzisha mpango mzuri wa soka vijana. 
    Alikuwa akichukua mipira yake mingi na kuwaita vijana, ili waonyeshe uwezo wao mbele ya macho yake. Waliomkuna kwa vipaji vyao aliwachukua na kwenda kuunda kikosi cha vijana kilichokuwa madhubuti cha klabu hiyo.
    Kwa mtaji huo, ndiyo walipatikana wanasoka nyota Tanzania kama Juma Pondamali 'Mensah', Mohamed Adolph Rishard, Mohamed Yahya 'Tostao', Kassim Manara, Mohamed Mkweche, Jaffar Abdulrahaman, Hamisi Swedi, Gordian Mapango na wengineo. 
    Wakati huo, Mwenyekiti wa Yanga alikuwa ni Mangara Tarbu (sasa marehemu).
    Baada ya Tambwe kutua Yanga, alitaka kufanya mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza, akitaka kutumia wachezaji vijana, akisema kwamba wakongwe uwezo wao unaelekea ukingoni. 
    Lakini ni kipindi hicho Yanga ilikuwa inatawala soka ya Tanzania, imetoka kutwaa ubingwa mfululizo tangu mwaka 1968 hadi 1972. 
    Mwaka 1973 watani wao wa jadi, Simba, ndio waliotwaa taji hilo, lakini mwaka 1974 Yanga walitwaa tena ubingwa wa nchi.
    Mwaka 1975, Yanga ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame, ikiifunga Simba kwenye fainali mabao 2-0 visiwani Zanzibar. 
    Wafungaji wa mabao hayo walikuwa wale wale wauaji wa fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa mwaka 1974, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu), katika ushindi wa 2-1, bao la Simba likifungwa na Adamu Sabu (sasa marehemu).
    Kwa sababu hiyo, ilikuwa ngumu kuwashawishi watu kwamba wachezaji wa Yanga wamezeeka.
    Kipindi hicho wakongwe wa Yanga walikuwa akina Elias Michael 'Nyoka Mweusi', Muhidini Fadhili na Patrick Nyaga, wote makipa, mabeki Boy Iddi Wickens, Athumani Kilambo 'Baba Watoto', Badi Saleh, Hassan Gobbos, Omar Kapera, viungo Abdurahman Juma, Abdurahman Lukongo, Sunday Manara 'Computer', Leonard Chitete, na washambuliaji Gibson Sembuli, Kitwana Manara 'Popat' na Maulid Dilunga.  
    Lakini pamoja na ubishi huo, baada ya kushindwa kutetea Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki mjini Mombasa, Kenya, uliibuka mgogoro mkubwa na wa kihistoria ndani ya klabu hiyo.
    Yanga ilianza vizuri tu katika kundi lake B, ikiifunga 2-1 Mseto SC ya Morogoro, kabla ya kuitandika Green Bufalloes ya Zambia 2-0, Bata Bullets ya Malawi 3-1, iliongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Mseto, mabingwa wa Tanzania mwaka 1975.
    Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga 3-0 Express ya Uganda wakati Mseto iliona cha mtema kuni kwa Luo, baada ya kutandikwa 5-0. Yanga iliuacha ubingwa Mombasa, baada ya kulala 2-1 kwa Luo kwenye fainali.
    Timu iliporejea nyumbani, mgogoro ukaibuka, wanachama walikuja juu na kutaka kumpiga Mwenyekiti wao wakati huo, mzee Mangara, ambaye aliokolewa kwa kutoroshewa mlango wa nyuma. 
    Vyanzo vinasema kwamba, wanachama walifika na bakora Jangwani wakitaka kumchapa Mangara. Walikuwa wanataka hesabu za mapato na matumizi ya klabu, lakini walikuwa wenye ghadhabu wakifanya fujo, hivyo ili kuepuka balaa hilo, Mangara alitoroshwa na kuwaacha ‘solemba’ waliokuwa wanamsubiri nje wamchape bakora. 
    Mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna Yanga kwa miaka minne.
    Kipindi hicho Yanga ilikuwa safi kiuchumi, ilikuwa ina mabasi matano yaliyokuwa yakiingizia fedha klabu, Uwanja wa Kaunda uliojengwa kwa mkopo wa Sh 500,000 wa Benki ya Nyumba (THB) ulikuwa bado mpya unavutia watu wengi wakati wa mazoezi ya timu hiyo.  
    Yanga ilisaidiwa pia fedha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Abeid Karume kiasi cha Sh milioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi.
    Aidha, Yanga ilikuwa ina mfadhili wake, aliyekuwa akiwasaidia fedha nyingi, Shiraz Sharrif, ingawa naye baada ya mgogoro alihamia Pan African, kwa sababu alikuwa ana imani na Mangara.
    Kutokana na jinsi Mangara alivyoishi vizuri na wachezaji wa klabu hiyo, alikuwa akiwapenda akiwafanya marafiki, basi wachezaji wote waliamua kumfuata na kuachana na Yanga. Walifikia hatua hiyo, baada ya jitihada za kushinikiza Mangara arejeshwe, ikiwemo kuandamana, kushindikana. Kwa jeuri, Yanga nayo ilisema acha waende na itaunda timu mpya.
    Hadi leo, ukiwauliza watu wa Yanga sababu za kugombana na mzee Mangara, wapo watakaosema wanachama walikuwa wakorofi na wengine watasema mzee huyo alikuwa akinufaika kwa kupitia mgongo wa Yanga.
    Katika sakata hilo, wachezaji wakongwe waliokuwa Yanga ili wasikae bure msimu wa 1976, walikwenda Morogoro kujiunga na klabu iliyokuwa ikiitwa Nyota Afrika, wakafanikiwa kuipandisha daraja, wakati wachezaji chipukizi awali walikwenda kujiunga na timu ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), iliyokuwa ikiitwa Breweries wakati huo.
    Lakini baadaye wachezaji waliokwenda Nyota walirejea Dar es Salaam kuungana na wadogo zao, kuanzisha timu iliyokuja kuwa tishio kwenye soka ya Tanzania, Pan African. Timu hiyo ilianzishwa chini ya Mangara, aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza klabu hiyo.
    Mbali na Mangara, wengine walioasisi timu hiyo ni Omar Muhajji, Sammy Mdee, Shiraz Sharrif, aliyekuwa mfadhili wa Yanga ambaye alihamishia noti zake kwa klabu ya Mtaa wa Swahili.
    Pan ilipata mashabiki wengi kwa sababu wengi waliokuwa wapenzi wa Yanga walihamia Pan. Walihamia kuwafuata wachezaji bora waliokuwa Yanga kuanzia wakongwe hadi chipukizi.
    Ni katika kipindi hicho, Yanga iliyumba sana na kupoteza makali yake katoka soka ya Tanzania. Haikuwa ajabu ilipotandikwa mabao 6-0 na watani wao wa jadi, Simba Julai 19, mwaka 1977.
    Wakati ikiwa katika harakati za kujiweka sawa, serikali ilitoa tamko la kuzuia makocha wa kigeni nchini, hivyo Tambwe Leya na aliyekuwa kocha wa Simba, Nabby Camara, raia wa Guinea aliyeifanya Simba icheze soka safi mno, waliondoka nchini.
    Baada ya miaka, Tambwe alirejea nchini mwishoni mwa mwaka 1994, lakini wakati huo aliikuta Yanga ipo chini ya kocha Nzoyisaba Tauzany kutoka Burundi, ambaye alikuwa anafanya vizuri.
    Wakati huo, Mwenyekiti wa Yanga Dk. Jabir Idrisa Katundu alimpokea vizuri Tambwe na wakajadiliana cha kufanya. Dk. Katundu akamuacha Tauzany aendelee na Yanga kubwa na Tambwe akapewa timu ya vijana, ambayo mwenyewe aliipa jina Black Star.
    Alikusanya vijana wenye vipaji na kuanza kuwapika ‘kimya kimya’ akaenda nao kwenye kambi ya Zanzibar kuwajenga kwa mazoezi ya fiziki kabla ya kuanza kuonyesha makali yake kwenye michezo ya kirafiki ikizifunga timu za huko.
    Black Star ya Tambwe ikaja kuwa timu ya kwanza ya Yanga mwaka mmoja tu baadaye ikiongezewa nguvu na wakongwe wachache waliokuwa chini ya Tauzany.
    Hiyo ilifuatia Yanga kuvunja tena kikosi mwaka 1994, baada ya kuwatuhumu wachezaji wake nyota kuhujumu mechi dhidi ya Simba timu ikafungwa 4-1. Ilidaiwa wachezaji wa Yanga walihongwa na mfadhili mmoja wa klabu hiyo aliyekuwa hapatani na uongozi wa klabu hiyo ili wafungishe kuukomoa uongozi. 
    Baadhi ya wachezaji waliobakizwa kikosini baada ya wengine nyota kama Said Mwamba ‘Kizota’, Salum Kabunda ‘Ninja’ (wote marehemu) kutupiwa virago ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote walitimuliwa kwa tuhuma hizo.
    Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili, ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh, Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan African.
    Haikuchukua muda kikosi cha yosso wa Yanga kikawa tishio hata kikaweza kufika Robo Fainali ya Kombe la Washindi barani Afrika, mwaka 1996 na kutolewa na Blackpool ya Zimbabwe. 
    Yosso hao wangeweza kufanya maajabu zaidi, kama si viongozi wakati huo kuendekeza imani za kishirikina na kuacha kuwapa maandalizi bora vijana, kwani wakihitaji ushindi wa 1-0 ili waingie Nusu Fainali kwenye mechi ya nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini, walijikuta wakifungwa tena 2-1 nyumbani.
    Mchezaji mmoja wa Yanga alifichua siri kwamba, wachezaji walibughudhiwa usiku kucha kwa mambo ya kishirikina na hawakulala vizuri, matokeo yake wakaamka wamechoka na kufungwa nyumbani.
    Awali, Yanga ilianza vyema kwa kuitoa Vaal Reef Professionals ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3, ikianza kulazimisha sare ya 2-2 ugenini, kabla ya kushinda 2-1 nyumbani.
    Katika raundi ya pili, Yanga ilikutana na Tamil Cadets Club ya Mauritius na kuitoa kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda ugenini  3-1 na kutoa sare ya 1-1 nyumbani, hivyo kukata tiketi ya Robo Fainali.
    Kwa nini nimemkumbuka Tambwe Leya? Wiki hii Yanga ilitambulisha wakuu wake wapya wa benchi la Ufundi, aliyekuwa kocha Mkuu Mholanzi, Hans van der Pluijm akihamia kwenye Ukurugenzi wa Ufundi na nafasi yake akimuacha Mzambia, George Lwandamina.
    Maofisa wengine katika benchi la Ufundi la Yanga wanabaki katika nafasi zao kama kabla ya mabadiliko haya.
    Baada tu ya tetesi za Pluijm kuhamishiwa kwenye Ukurugenzi, binafsi nilimuuliza kama atakuwa tayari kwa majukumu mapya, na majibu yake yalikuwa; “Sipendelei hiyo kazi. Nataka kufanya kazi na wachezaji kila siku kwa matakwa ya moyo wangu,”alisema.
    Na Pluijm kwa hiari yake alitaka kuondoka Yanga, ila baada ya kubembelezwa na klabu na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba shabiki wa klabu hiyo, amekubali kubaki katika majukumu mapya.
    Lakini kimsingi Pluijm hajakubali Ukurugenzi wa Ufundi kwa utashi wake, bali shinikizo la klabu. Najiuliza kwa nini Yanga isimpe Pluijm kitu anachopenda, ambacho ni kufundisha wachezaji?
    Naona ni wakati mwafaka sasa Yanga kuwa na programu rasmi ya vijana kwa kumpa majukumu ya timu ya vijana Pluijm na anaweza akawasaidia kuwazalishia vipaji vizuri na kuwaepushia matumizi ya fedha nyingi za kusajili kila dirisha linapowadia.
    Yanga ikimtumia vizuri Pluijm itatamani kuendelea kuwa naye milele, lakini kwa kumlazimisha nafasi ya Ukurugenzi sitarajii kama atakuwa na maisha marefu Jangwani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA IKIMTUMIA KWA FAIDA PLUIJM ITATAMANI KUWA NAYE DAIMA MILELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top