• HABARI MPYA

  Tuesday, December 15, 2015

  HANS POPPE: MSIMU HUU LAZIMA TUCHUKUE KOMBE TURUDI MICHUANO YA AFRIKA 2017

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amewataka mashabiki wa timu hiyo wajiandae kuishangilia tena timu yao katika michuano ya Afrika mwaka 2017.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Poppe amesema kwamba pamoja na mazingira magumu wanayokabiliana nayo hivi sasa, lakini watahakikisha wanapata tiketi ya kurudi kwenye michuano ya Afrika mwaka 2017.
  “Hadi sasa kwenye Ligi Kuu mwenendo wetu si mbaya, tuna nafasi ya kuchukua ubingwa. Lakini pia tunajipanga vizuri kwa ajili ya michuano ya Kombe la TFF, ili tuchukue ubingwa,”amesema.
  Zacharia Hans Poppe amesema kwamba msimu huu lazima wachukue Kombe

  Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara hucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika, wakati bingwa wa Kombe la Azam HD TFF atacheza Kombe la Shirikisho kuanzia mwaka 2017.
  Na Poppe amesema kwamba baada ya miaka mitatu ya kuwa nje ya michuano ya Afrika, sasa wamepania kurudi.
  “Na kama historia inavyoonyesha, Simba SC ikipotea kwa muda mrefu kwenye michuano ya Afrika inarudi kwa nguvu na kuweka rekodi, sasa tunaomba wana Simba wawe na subira, 2017 siyo mbali,”amesema.
  Poppe amesema kwamba sasa uongozi wa Simba SC umeunganisha nguvu na wachezaji na makocha wao ili kuhakikisha kwa pamoja wanapambana hadi dakika ya mwisho wavune kitu.
  “Hatutaki kujivuruga wala kuvurugwa safari hii, tumejifunza kutokana na makosa na sasa tumetulia ili mwisho wa msimu tuvune kitu. Tuna kiu ya kurudi kwenye michuano ya Afrika,”amesema. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: MSIMU HUU LAZIMA TUCHUKUE KOMBE TURUDI MICHUANO YA AFRIKA 2017 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top