• HABARI MPYA

    Wednesday, December 30, 2015

    AZAM YAIPOKONYA YANGA ‘KITI CHA UFALME’ LIGI KUU, BOCCO AWAANGAMIZA MTIBWA SUGAR CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAO la Nahodha John Raphael Bocco (pichani kushoto) dakika ya 86, limeirejesha Azam FC kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni ya leo.
    Ushindi huo, unaifanya timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ifikishe pointi 35, baada ya kucheza mechi 13 sasa wakiwazidi kwa pointi mbili mabingwa watetezi, Yanga SC.
    Bocco maarufu kwa jina la utani ‘Adebayor’, alifunga bao zuri kwa shuti la mpira wa adhabu nje kidogo ya boksi, kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa na beki wa Mtibwa, Salum Mbonde kwenye duara la nje ya 18.
    Wachezaji wa Mtibwa itabidi wajilaumu wenyewe kwa kutojipanga vizuri wakati Bocco anapiga mpira huo, kiasi cha kumpoteza kipa wao, Said Mohammed hata akafungwa kwa urahisi. 
    Mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbangu akiwatoka wachezaji wa Mtibwa Sugar
    Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza Bocco baada ya kufunga leo

    Kwa ujumla mchezo wa leo ulikuwa mkali na wa kusisimua na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
    Mshambuliaji Mrundi wa Azam FC, Didier Kavumbangu alipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 10 baada ya kuunganishia nje krosi ya Bocco. Kavumbangu anaye alimsetia vizuri Bocco dakika ya 12, lakini akashindwa kufunga.
    Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Said Bahanuzi alikaribia kufunga dakika ya 27 kama si shuti lake kupanguliwa na kipa wa Azam FC, Aishi Manula na dakika ya 34 Shizza Kichuya naye alikaribia kufunga kwa shuti kali kutoka nje ya boksi kama si kipa wa Azam kudaka.
    Ligi Kuu itaendelea keshokutwa kwa mchezo mmoja kati ya Ndanda FC na Simba SC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara na baada ya hapo kutakuwa na mapumziko mafupi hadi katikati ya Januari. 
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Abdallah Kheri, Racine Diouf, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco, Didier Kavumbagu/Kipre Tchetche dk62 na Farid Mussa/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk55. 
    Mtibwa Sugar; Said Muhammed, Ally Shomari, Issa Rashid, Salim Mbonde, Andrew Vicent, Henry Joseph, Said Bahanuzi/Jaffar Salum dk60, Mzamiro Yassin, Boniface Maganga, Mohammed Ibrahim/Ibrahim Rajab dk82 na Shizza Kichuya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAIPOKONYA YANGA ‘KITI CHA UFALME’ LIGI KUU, BOCCO AWAANGAMIZA MTIBWA SUGAR CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top