• HABARI MPYA

    Wednesday, December 16, 2015

    KAMUSOKO AIREJESHA YANGA SC KILELENI LIGI KUU

    Kiungo mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko ameirejesha Yanga SC kileleni keo baada ya kufunga bao pekee dhidi ya African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
    Na Mohammed Slim, TANGA
    YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
    Shukrani kwake, kiungo wa kimataifa wa Zimbabwe, Thabani Scara Kamusoko aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 90 na ushei na kuwarejesha wana Jangwani hao kileleni.
    Kamusoko alifunga bao hilo kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kichwa ya Mzimbabwe mwenzake, Donald Dombo Ngoma ambaye naye alipokea krosi ya winga Godfrey Mwashiuya.
    Na kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 27, baada ya kucheza mechi 11, ikiizidi pointi moja Azam FC yenye mechi moja mkononi, ambayo sasa inashukia nafasi ya pili.
    Mchezo wa leo ulikuwa mgumu haswa kwa Yanga SC na ilibaki kidogo tu itoe sare ya pili mfululizo Uwanja wa Mkwakwani, baada ya Jumamosi kulazimishwa sare ya 0-0 na Mgambo JKT.
    Mshambuliaji wa Yanga SC, Donald Ngoma akipasua katikati ya wachezaji wa African Sports leo

    Ni mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm yaliyoisaidia Yanga SC kuongeza kasi ya mashambulizi hadi kupata bao.
    Pluijm anayesaidiwa na mzalendo, Juma Mwambusi aliwatoa washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Deus Kaseke dakika za mwishonin na kuwaingiza Malimi Busungu na Mwashiuya waliokwenda kuipasua ngome ya Sports. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Deus Kaseke/ Godfrey Mwashiuya.
    African Sports; Ramadhani Mwaluko, Mwaita Ngereza, Khalfan Twenye, Juma Shemvuni, Rahim Juma, Mussa Chambega/Ally Ramadhani ‘Kagawa’,
    Mussa Kizenga/James Mendi, Pera Ramadhani, Hassan Materema, Mohammed Mtindi/Hussein Issa na Mohamed Issa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMUSOKO AIREJESHA YANGA SC KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top