• HABARI MPYA

    Wednesday, December 30, 2015

    MALINZI: 2016 UTAKUWA MWAKA WA MAFANIKIO KWA SOKA YA TANZANIA

    "Ndugu zangu, Kwa niaba ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia kwenu wanahabari ninaomba nitoe salam za mwaka za Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF.
    Awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametulinda kwa mwaka mzima na kupitia Baraka zake tumeweza kuwa na nguvu, uwezo na hekima za kutimiza majukumu yetu mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2015. Tuzidi kumuomba atuvushe salama mwaka 2015.
    Ninaomba nichukue fursa hii kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Ninampongeza Mh. Dr John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hongera sana Mama Samia Suluhu kwa kuwa Makamu wa Rais na hongera kwa mwanamichezo mwenzetu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kushinda ubunge jimbo la Ruangwa na kwa uteuzi wa kuwa Waziri wetu Mkuu. Hongera za kipekee kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kwa uteuzi wa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na hongera pia kwa Mama Anastasia Wambura kwa kuteuliwa kuwa naibu waziri wa wizara hii muhimu kwa mustakabali wa afya na ajira kwa vijana na utangazaji wa jina la Nchi yetu ya Tanzania nje ya mipaka ya nchi. Ninashukuru Mh. Waziri Nnauye majuzi alinipatia fursa ya kuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa vyama vya Kitaifa vya michezo ya kukutana naye na kujitambulisha rasmi kwake, ahsante sana.
    Ndugu zangu, Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu Tanzania. Tunafanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wote wapenzi wa mpira wa miguu. Kwa kutambua uzito na umuhimu wa jukumu hili ndio maana wakati wote TFF inafanya jitihada za dhati kuhakikisha timu zetu za Taifa zinafanya vizuri. Kwa sasa tunazo timu za Taifa kumi ambazo ni za soka la ufukweni wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 17 wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 20 wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 23 wanawake na wanaume na mbili za wakubwa za wanawake na wanaume.  Katika kuingiza timu kwenye mashindano ya kimataifa tumekuwa tukizingatia vigezo kadhaa lakini kikubwa ikiwa ni utayari wa timu kushiriki mashindano na uwezo wa kugharamia mchezo wenyewe. Kwa wastani gharama za kushiriki mkondo mmoja wa mechi ya Kimataifa kwa kucheza nyumbani na ugenini ni takribani shilingi million mia moja (USD 50,000.-), hii inajumuisha gharama za kambi, usafiri kwenda ugenini, posho, nauli na posho za waamuzi na kamisaa, malazi ya waamuzi na kamisaa nk. Kwa kuwa timu yenye udhamini kwa sasa ni timu ya Taifa wanaume tuu hivyo TFF imekuwa inabeba yenyewe gharama nyingine zote kwa timu zote zilizobakia. Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utashuhudia ufadhili unapatikana kwa timu zetu nyingine za Taifa.
    Ninaomba sasa nichukue fursa hii kuzungumzia maeneo kadhaa ambayo yamehusu mpira wetu na taasisi yetu kwa mwaka 2015:
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi (katikati) wakati wa kutangazwa kwa udhamini wa Azam TV Ligi Daraja la Kwanza

    1.   Timu ya Taifa ya wanaume “Taifa Stars”
    Baada ya timu yetu ya Taifa, Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini mwezi Mei mwaka huu na baadae kufuatia kufanya vibaya katika mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN, Kamati ya Utendaji ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni Martin Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wamechukua timu ya Taifa Stars tumefungwa mechi mbili tuu za mashindano dhidi ya Algeria na Malawi ugenini, tumetoka sare na Uganda ugenini, tumetoka sare na Nigeria na Algeria nyumbani na kuwafunga Malawi nyumbani. Aidha timu ya Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi wake Juma Mgunda katika mashindano ya CECAFA  Challenge katika mechi nne ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja kwa muda wa mchezo (Open Play) ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu fainali. Katika mashindano hayo Taifa Stars ilishinda mechi mbili na kutoka sare mbili. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha hawa wazawa kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza sana makocha wetu hawa na benchi zima la ufundi. Kwa sasa tunajiandaa na mechi mbali mbali za kufuzu kucheza fainali za Afrika Afcon 2017 nchini Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 25/03/2016 ugenini Ndjadema na mechi ya marudiano siku tatu baadae hapa Dar es Salaam tarehe 28/03/2015. Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi. Katika kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria, Taifa Stars iliweka kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili. Katika kujiandaa na mechi dhidi ya Tchadi mwezi Machi mwakani ratiba ya ligi kuu ikiruhusu timu itaweka kambi pia nje ya nchi.
    Wachezaji wa Taifa Stars kabla ya mchezo na Nigeria Dar es Salaam

    2.   Timu ya Taifa Wanawake “Twiga Stars”.
    Timu yetu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage ilifanikiwa kuiondoa Zambia na hivyo kufuzu fainali za michezo ya Afrika Kusini Kongo Brazaville. Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa kaika hatua za makundi. Tunaamini uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo utaimarisha timu na kufanya Twiga Stars iweze kushiriki fainali ya Afrika ya mpira wa wanawake nchini Cameroon mwaka 2016.
    Hatua ya awali Tanzania itapambana na Zimbabwe mwezi Machi 2016 na mshindi wa michezo huo atacheza hatua ya pili dhidi ya mshindi kati ya Namibia na Zambia.

    3.   Udhamini na michuano mipya.
    Kwa kipindi hiki cha mwaka 2015 tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:

    3.1  Kufufua Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation Cup.
    Kwa kushirikiana na mdhamini Azam Sports Kombe la Shirikisho limefufuliwa na kuboreshwa. Kwa mwaka huu tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi kuu (16), Ligi daraja la kwanza FDL (24) na Ligi daraja la pili SDL (24). Ili kupanua uwigo wa ushiriki wa Mikoa yote kwa misimu ya usoni timu mabingwa wa mikoa (RCL) nazo zitashirikishwa katika mashindano haya ili kila mkoa wa Tanzania upate fursa ya kushiriki katika mashindano haya. Fainali itachezwa mwezi Mei na bingwa wa Kombe hili ataiwakilisha Tanzania katika kombe la Shirikisho la Afrika CAF Confederation Cup.

    3.2   Udhamini Ligi daraja la kwanza.
    Tumefanikiwa kupata wadhamini wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata STARTIMES ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni ya Television ya Sahara Media kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha mechi hizi moja kwa moja. Haya ni mafanikio makubwa kwa ligi ya daraja la kwanza. Tunaishukuru kampuni ya Geita Gold kwa kuidhamini timu ya daraja la kwanza ya Geita Gold Sport na tunazidi kutoa wito kwa washirika wengine wazidi kujitokeza kudhamini timu zetu.

    3.3    Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.
    Kampuni ya Vodacom baada ya mazungumzo marefu tuliafikiana na kutuliana saini ya mkataba mwingine wa miaka mitatu wa udhamini wa ligi kuu wenye ongezeko la thamani ya udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika kuvutia wadhamini wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu. Tunaishukuru kampuni ya ACACIA ambayo imejitolea kuidhamini klabu ya ligi kuu ya Stand United haya ni mafanikio makubwa kwa ligi yetu na tunazidi kuvipa moyo vilabu vizidi kupata wadhamini zaidi. Tunayashukuru sana makampuni yote ambayo yamejitokeza kudhamini vilabu mbali mbali na tunazidi kutoa wito kwa makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini ikiwa ni sehemu ya kutangaza biashara na kukuza jina la chapa zao.

    3.4   Udhamini tarajiwa.
    Tunatarajia kupata wadhamini kwa ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) pamoja na ligi kya vilabu vya ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U-20).
    Jambo hili likifanikiwa matumaini yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili mwaka 2016, Ligi ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) na ligi ya vilabu vya ligi kuu ya vijana umri chini ya miaka 20 (U-20). Mechi hizi nazo zitakuwa zinaonyeshwa moja kwa moja kwenye television.
    Kwa matarajio haya sasa ni vyema uongozi wa kila mkoa kufanya jitihada za kuhakikisha vilabu vya mpira vya wanawake vinaanzishwa ili tuweze kuwa na ligi ya ushindani.
    Ninaomba nichukue fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote, ambao kama sio kujitolea kwa haya mafanikio tusingeweza kuyafikia/kuyapata.
    Ahsante Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia bia ya Kilimanjaro Lager.
    Ahsante Vodacom.
    Ahsante Azam Tv kwa kupitia channel ya Azam Sports HD.
    Ahsante Startimes Media kwa kupitia king’amuzi cha STARTIMES.
    Ahsante Sahara Media kwa kupitia Star Tv.
    Ahsante AIRTEL kwa kutuletea Airtel Raising Star kwa mara nyingine mwaka huu.
    Ahsante Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF.

    4.   Soka la Vijana.
    Kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 15

    4.1   Fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2017 Madagascar.
    Kikosi chetu cha Taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kinachojiandaa na hatua za mtoano mwezi Juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara ya kimichezo katika nchi za Rwanda, Uganda na Kenya, lengo ilikuwa kuwapatia vijana hao uzoefu wa Kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na kukabidhiwa bendera, akaunti za TFF zilifungiwa na mamlaka za mapato TRA na hivyo safari kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Mpango mkakati ni kuwa mwezi Aprili, 2016 timu hii itaweka kambi nje ya nchi ili kujiandaa na hatua ya mtoano (qualifiers).

    4.2  Fainali za Afrika U-17 mwaka 2019.
    Maandalizi ya fainali hizi ambazo Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri vikao na Wizara tayari vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya awali ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya timu itakayoshiriki fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13 (U-13) kujumuishwa pamoja katika shule ya Alliance jijini Mwanza. Imani yetu ni kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia kunyakua kombe hili.

    4.3   Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.
    Azma ya TFF ni kuhakikisha kuwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa na kituo mama cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira. Mkataba wa mfano (template) umekwisha pelekwa katika kila mkoa ili vyama vya mkoa ambavyo havina vituo vyake basi viingie mkataba wa ushirikiano na kituo kimoja kwa lengo la kukifanya kiwe kituo mama cha mkoa. Kupitia vituo hivi TFF itaweza kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa yetu, kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na walimu. Mipira 5,000 ya 3 na 4 ya ukubwa (size), koni 3,000, beeps 2,000 tayari vimeagizwa toka nje ya nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada kutoka popote kwa ajili ya kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una mwalimu angalau mmoja aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha wa vijana isipokuwa mikoa miwili tu ya Manyara na Njombe, jitihada zitafanyika nao wapate walimu stahiki. Hivyo mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo hivi. Pindi vituo hivi vikiimarika yataanzishwa mashindano ya kiumri (age categories) baina ya vituo hivi kuanzia ngazi ya mkoa, kanda na hatimaye Taifa. Ninatoa wito kwa viongozi wenzangu  wa mikoa tujizatiti tuweke nguvu katika uwanzishwaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo vitakuwa chachu kuu ya kutoa wachezaji  wa Taifa wa kike na wakiume. Baada ya mazungumzo haya nitawakabidhi viongozi wa vyama vya mpira vya mkoa wa Manyara na Dar es Salaam mpira mmoja mmoja ikiwa ni ishara ya kuanzishwa rasmi kwa program hii ya kitaifa.

    5.  Kozi mbalimbali.
    Kwa kushirikiana na CAF na FIFA Shirikisho letu limeandaa, kuratibu na kutoa kozi mbali mbali za waamuzi na makocha katika ngazi mbalimbali. Jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo ya makocha na waamuzi inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru viongozi wote wa mikoa na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma hii. Juhudi zinaendelea ili tuweze kupata makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na watawala zaidi. Ninaomba tuwape moyo wakina mama wazidi kujitokeza kwa wingi kufanya kozi hizi maana wao ndio nguzo kuu ya kuendeleza mpira wa wanawake nchini mwetu. Ninatoa rai kwa waajiri, hasa wakurugenzi wa Halmashauri ambao ni waajiri wa walimu wanaofundisha mpira mashuleni, wazidi kutupatia ushirikiano kwa kutoa ruhusa kwa waajiriwa wao pindi wanapoomba kuhudhuria kozi mbalimbali zitolewazo na TFF.

    6.   Bodi ya Ligi na Vilabu.
    Utendaji katika bodi yetu umeimarishwa kwa kutoa ajira kwa mtendaji mkuu Ndugu Boniface Wambura. Mipango ya kuimarisha sekretariet ya Bodi ikiwa ni pamoja na kupata nafasi kubwa zaidi ya kufanyia kazi iko mbioni. Matarajio yetu ni kuwa chombo hiki kikiweza kuimarika kitakuwa ni chachu ya kuandaa ligi zilizo bora zaidi na zenye ushindani.
    Pamoja na jitihada za kutafuta wadhamini wa mashindano mbalimbali yanayohusisha vilabu, jitihada pia zinaendelea kufanyika kuhakikisha vilabu vyetu vinaimarisha utawala bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu (Club Licencing) jitihada sasa zinafanyika kuhakikisha vilabu vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya leseni hizi. Katika utaratibu wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa vitalazimika kuwa na ofisi, watendaji wa kuajiriwa, kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi, kuwa na program ya maendeleo ya vijana, kuajiri walimu wenye sifa n.k. Tunaamini utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo uendeshaji wa vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu vyetu.

    7.   Tiketi za Eletroniki.
    Kutokana na matatizo yaliyojitokeza matumizi ya tiketi za eletroniki yalisimamishwa na mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada ya mazungumzo na mtoa huduma ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa atafutwe mshauri mwelekezi (Consultant) kwa kupitia mfumo mzima ili kubaini matatizo na baadae kutoa ushauri wa namna ya kuboresha mfumo huo. Tenda ya kumpata mshauri huyu ilikwishatangazwa na kinachofuatia ni TFF kwa kushirikiana na CRDB kuteua mshauri huyo. Imani yetu ni kuwa kazi ya mshauri ikikamilika basi mwongozo utapatikana ili utekelezaji wa uboreshaji wa mfumo ukamilike na matumizi ya tiketi za eletroniki yaweze kuendelea.

    8.   Mfuko wa Maendeleo ya Mpira (Football Development Fund).
    Baada ya mfuko huu kuanzishwa kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya utendaji ya TFF iliteua wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko huu chini ya Mwenyekiti Ndugu Tido Mhando na Mtendaji Mkuu Henry Tandau. Mfuko huu tayari umefanikiwa kupata ofisi yake na shughuli zake zitaanza punde baada ya kuwekewa vitendea kazi. Lengo la mfuko huu kama ilivyoanishwa ni kuwa chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na kuwapa ushirikiano watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo ya mpira yanahitaji rasilimali nyingi.

    9.   Kufungiwa akaunti za TFF.
    Kutokana na madeni ambayo yamekuwa kwenye mafaili ya mamlaka ya mapato kwa kipindi karibia miaka mitano iliyopita, mamlaka ya mapato nchini TRA iliamua kuzifungia akaunti zetu na pesa yote kuhamishiwa Benki kuu. Mazungumzo yanaendelea kati ya TFF, Mamlaka ya mapato na Wizara husika ili fedha hizi ziweze kurudishwa. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao wametusaidia kutuongoza namna ya kukabiliana na changamoto hii.

    OMBI  KWA SERIKALI.
    Duniani kote, iwe katika nchi tajiri au maskini, michezo huendelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na taasisi zinazoendesha shughuli za michezo husika. Tunaiomba serikali tuzidi kushirikiana kwa karibu katika kuandaa timu zetu za Taifa, kuboresha miundo mbinu ya kuchezea mpira, kusaidia upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa gharama nafuu, kuto fursa kwa waajiriwa wake, hasa walimu, wafanye kozi mbalimbali za ukocha na uamuzi. TFF itafarikika sana iwapo itapewa fursa na Serikali ya kuratibu na kusimamia mpira wa miguu katika mashindano ya Taifa ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA). Tunaamini TFF ikipewa fursa hiyo itaongeza uweledi katika usimamizi wa mashindano hayo na kuhakikisha vipaji vinaibuliwa kila mwaka kuliko ilivyo sasa.
    Ndugu zangu, wakati tunauaga mwaka 2015 na kuelekea kuingia mwaka 2016 ninaomba nimalizie kwa kutoa wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania tuzidi kushirikiana, penye makosa tukosoane japo kwa staha na penye kuhitaji ushauri tushauriane.
    Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mpira wetu".

    (Mungu Ibariki Tanzania. Mungu Ibariki Afrika. Ahsanteni, Jamal Malinzi, Rais wa TFF Dar es Salaam. 30 Desemba, 2015)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI: 2016 UTAKUWA MWAKA WA MAFANIKIO KWA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top