• HABARI MPYA

    Monday, December 21, 2015

    SIMBA SC YAMSHUSHIA ‘RUNGU ZITO’ MAJABVI, YAMKATA MSHAHARA, ADHABU MYINGINE YAJA

    Na Princess Asia, MWANZA
    KIUNGO Mzimbabwe, Justive Majabvi amekatwa mshahara kwa kitendo cha kuzungumza na vyombo vya Habari, jambo ambalo ni kinyume cha Mkataba wake.
    Aidha, mchezaji huyo pia anatarajiwa kupewa adhabu nyingine, kwa kitendo cha kutoonekana kwenye mazoezi kwa zaidi ya wiki mbili.
    Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe katika mazungumzo na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana mjini Mwanza, ambako juzi timu hiyo ililazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji Toto Africans katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.  
    Kiungo Justive Majabvi (kushoto) amekatwa mshahara kwa kuzungumza na vyombo vya Habari, wakati adhabu nyingine inakuja kwa kutoonekana mazoezi zaidi ya wiki mbili
     

    “Tunaposema aende zake, maana yake tuko tayari kuvunja mkataba wake na maadamu yeye ndiye anataka kufanya hivyo, kuna mambo ambayo lazima atekeleze ambayo ni kuilipa klabu kwa mujibu wa katiba,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). “Kwa sasa amekatwa mshahara kwa kuongea na vyombo vya habari na kwa kutokuwa kambini ana adhabu yake,” ameongeza. 
    Majabvi hayupo kambini kwa zaidi ya wiki mbili Simba SC, baada ya kutofautiana na uongozi kiasi cha kufikia kusema haridhishwi timu inavyoendeshwa na hajisikii kuendelea kucheza Msimbazi.
    Lakini Simba SC inaamini mchezaji wake huyo anarubuniwa na moja ya klabu wapinzani wao avunje Mkataba ili wamchukue – na Poppe amesema Majabvi amenza visa ambavyo wazi inaonyesha anataka kuvunja Mkataba.
    “Kuna wapinzani wetu fulani, ambao kwa sasa wapo kwenye mgogoro na mchezaji wao mmoja, sasa wamemrubuni na huyu wa kwetu ili wamchukue badala ya huyo anayewasumbua,”amesema Poppe.
    Kwa ujumla, Simba SC ipo tayari kumuacha Majabvi aondoke iwapo atafuata taratibu za kuvunja Mkataba wake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAMSHUSHIA ‘RUNGU ZITO’ MAJABVI, YAMKATA MSHAHARA, ADHABU MYINGINE YAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top