• HABARI MPYA

    Wednesday, December 30, 2015

    NATAMANI YANGA WAMSAMEHE, LAKINI NAPENDA NAYE ABADILIKE

    BINAFSI bado sijaamini kama kiungo mtaalamu Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amevunjiwa Mkataba Yanga SC.
    Nadhani kama anatikiswa, lakini mwishowe atasamehewa – ili kumshikisha adabu na kutoa onyo kwa wachezaji wengine pia waheshimu mikataba yao na klabu.
    Naam, gumzo kubwa katika soka ya Tanzania kwa sasa ni sakata la Yanga kiungo wake wa kimataifa wa Rwanda, Niyonzima.
    Yanga SC juzi imetangaza kuvunja Mkataba na kiungo wake, Nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda kwa madai ya mchezaji huyo wa Amavubi kukiuka vipengele.

    Sakata la kufukuzwa kwa Niyonzima Yanga SC, linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.
    Kufuatia hali hiyo, klabu ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.
    Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.  
    Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
    Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
    Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
    Na tangu ametua Yanga SC kwa kweli amekuwa mchezaji kipenzi cha wapenzi wa timu hiyo na tegemeo la timu kwa ujumla.
    Huwezi kumtenganisha Niyonzima na mafanikio ya Yanga SC katika kipindi cha miaka mitano hii, ikiwemo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
    Mimi, binafsi ni shabiki wa Niyonzima na alipokuja nchini nilikuwa mwandishi wa kwanza kufanya naye mahojiano na kuandika makala gazetini.
    Lakini pamoja na ukweli huo, siwezi kuunga mkono aina yoyote ya utovu wa nidhamu kwa mchezaji yeyote – si yeye tu Haruna.
    Nchi hii nimekwishaingia kwenye ugomvi na wachezaji wengi tu kwa kuandika kulaani vitendo vyao vya utovu wa nidhamu. Ila baadaye wengine walipojitambua, walikiri niliwasaidia kuwashitua, walikuwa wanapotea.
    Siku zote nawaambia wachezaji wa Tanzania wasiwaone Waafrika wenzao wanaogelea kwenye mabwawa ya fedha ya klabu za Ulaya wakadhani walifika huko kwa urahisi.
    Hapana, juhudi za mazoezi, nidhamu na kutilia mkazo malengo bila kukata tamaa au kuridhika kwa mafanikio ya awali ndivyo huwafikisha huko.
    Kama Victor Wanyama angeridhika na mafanikio ya awali, leo asingekuwa mchezaji wa klabu ya Ligi Kuu England – lazima alibaki kuwa mwenye nidhamu, juhudi za mazoezi na malengo ya kufika mbali zaidi.
    Hayo ndiyo mambo ambayo wachezaji wa huku kwetu wanakosa – na wala si vipaji. Kwa vipaji tu, wengi wanavyo na ndiyo maana wanaitana fundi.
    Kama mshahara wa dola za Kimarekani 3,000 (Sh. Milioni 6) unakutia wazimu na kujiona umemaliza, vipi utafikia kulipwa dola 100,000 (Milioni 200 na ziadi) kwa wiki?
    Na kwa muda mrefu klabu zetu nchini zimeshindwa kutusaidia katika vita ya kuwanyoosha wachezaji wetu kutokana na kuwaabudu kupita kiasi hata pale wanapopotoka.
    Kilichofanywa na Yanga SC lazima kiungwe mkono na klabu nyingine nchini, ili kila mchezaji mwenye Mkataba na timu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara auheshimu.
    Lakini kwa muda mrefu imekuwa vigumu kwa sababu mchezaji anapoharibu Simba, Yanga wanamsajili. Na anapoharibu Yanga, Simba wanamsajili – klabu zenyewe zikiamini zinakomoana, kumbe zinajikomoa zenyewe.     
    Inasikitisha sana kwa kweli, kwa sababu mwisho wa siku soka ndiyo ajira ya vijana wetu na hatupendi waharibu mambo yao, lakini inapobidi kuadabishwa tunapaswa kukubaliana na hali halisi. 
    Nampenda Niyonzima na kama ambavyo naamini Yanga SC wanamtikisa naomba iwe hivyo. Lakini pia ninaomba naye ajitambue na abadilike.
    Namkumbuka Haruna yule ambaye wakati anawasili Dar es Salaam alikuwa mtu wa sala tano, kijana mpole na mwenye nidhamu ya ndani na nje ya Uwanja.
    Ni tofauti na Haruna huyu wa sasa ambao sisiti kusema amekuwa mtu wa anasa kiasi cha hata kuchangia kushusha kiwango chake. 
    Natamani Yanga SC wamsamehe Haruna. Lakini napenda na mchezaji mwenyewe ajirudi na kurejea kuwa yule ambaye tulimpokea Dar es Salaam mwaka 2011. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NATAMANI YANGA WAMSAMEHE, LAKINI NAPENDA NAYE ABADILIKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top