• HABARI MPYA

  Sunday, November 04, 2018

  WAKATI UMEFIKA IBRAHIM AJIB AANZE KUFANYIA KAZI ANAYOAMBIWA NA MAKOCHA WAKE

  ANAFANYA vizuri katika klabu yake na kwa sasa ndiye mchezaji tegemeo zaidi Yanga SC.
  Namzungumzia Ibrahim Ajib Migomba, kiungo mshambauliaji aliye katika msimu wa pili Yanga SC tangu asajiliwe kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
  Baada ya kukosekana mara mbili katika vikosi vya timu ya taifa vya kocha mpya, Mnigeria, Emmanuel Amunike safari hii Ajib alitarajiwa sana kupewa nafasi. 
  Lakini kwa mara nyingine, jicho la Amunike bado halipendezewa na kiungo huyo anayeweza kucheza pia kama mshambuliaji,  japokuwa Taifa Stars itamkosa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano.

  Pamoja na hayo, winga huyo wa zamani wa Barcelona na Nigeria, Amunike ameimarisha safu yake ya kiungo kwa kumchukua Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuziba pengo la kiungo mwenzake wa Azam FC, Frank Domayo ambaye majeruhi pia.
  Amemuita pia kiungo Shiza Ramadhani Kichuya katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
  Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na Amunike baada ya kumpuuza katika mechi tatu zilizopita Kichuya, sasa amempa nafasi.
  Kwa kiasi kikubwa Amunike amerejesha kikosi kilichompa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 mjini Dar es Salaam kikitoka kuchapwa 3-0 mjini Praia na Papa wa Bluu Oktoba 12.
  Makipa ni; Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
  Mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
  Viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum KImenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani.
  Washambuliaji ni Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
  Kikosi hicho chini ya makocha Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
  Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
  Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
  Ukirejea uwezo aliounyesha siku za karibuni unaweza ukajiuliza mara mbili, kwa nini Amunike hajamchukua Ajib.
  Ni kweli Tanzania ina wachezaji wengi wa aina ya Ajib, isipokuwa wanazidiana vitu vichache tu na vitu vingi alivyonavyo, au anavyofanya mchezaji huyo wa Yanga ‘Mtoto wa Mjini’ si kipaumbele cha makocha wengi wataka ushindi.
  Ni mchezaji mzuri ukiwa naye kikosini na utapenda kumchezesha kwa sababu ya vitu vyake, ila linapokuja suala ya nidhamu ya uwajibikaji uwanjani na kucheza kwa maelekezo ya kocha, unaweza kuwapa nafasi wachezaji wengine mbele ya Ajib – na ndicho kinachotokea kwa sasa kwa Amunike.
  Naamini Amunike anamuona Ajib na anavutiwa na vitu vingi anavofanya kwa sababu Nigeria ni waumini wa soka ya madoido anayoicheza Ajib – si ndiyo nchi ambayo anatokea Augustine Azuka ‘Jay-Jay’ Okocha, lakini si aina ya wachezaji anaowahitaji sasa akipigania kuipa Tanzania tiketi ya kwanza ya AFCON baada ya miaka 38.
  Ukirejea namba alivyoondoka Simba SC, ni kwa sababu kama hizi zinazoonekana kwa sasa Yanga, mchezaji mzuri lakini umuhimu wake hauonekani.
  Desemba 9 mwaka huu atafikisha miaka 22 tangu azaliwe, bado ni kijana mdogo na ana nafasi kubwa ya kubadilika kwa kusikiliza ushauri wa makocha wake ili awe aina ya mchezaji atakayemvutia kocha yoyote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAKATI UMEFIKA IBRAHIM AJIB AANZE KUFANYIA KAZI ANAYOAMBIWA NA MAKOCHA WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top