• HABARI MPYA

    Sunday, November 04, 2018

    KICHUYA NA SURE BOY WALIKUWA WANAKOSEKANA STARS VITA YA KUWANIA TIKETI YA AFCON 2019

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mnigeria, Emmanuel Amunike ametaja kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
    Amunike ameongeza wachezaji wawili tu, viungo Shiza Kichuya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ katika kikosi hicho cha Taifa Stars ambacho kitamfuata  Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani.
    Bila shaka, Kichuya ni mbadala wa Farid Mussa wa timu B CD Tenerife ya Hispania ambaye kwa sasa kidogo kiwango chake kimeshuka kutokana na kukosa mechi za ushindani kama ilivyokuwa nyumbani, ingawa anajengwa vizuri zaidi kisoka Ulaya.

    Shiza Kichuya ni mchezaji aliyekuwa anakosekana Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike

    Na hapana shaka winga huyo wa zamani wa Barcelona na Nigeria, Amunike amemchukua Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kuziba pengo la kiungo mwenzake wa Azam FC, Frank Domayo ambaye majeruhi pia.
    Kwa kiasi kikubwa Amunike amerejesha kikosi kilichompa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 mjini Dar es Salaam kikitoka kuchapwa 3-0 mjini Praia na Papa wa Bluu Oktoba 12.
    Makipa ni; Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
    Mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
    Viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum KImenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani.
    Washambuliaji ni Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   

    Salum Abubakar 'Sure Boy' (kulia) ni mchezaji aliyekuwa anakosekana Taifa Stars

    Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
    Katika mechi na Cape Verde mjini Dar es Salaam, ilionekana wazi Taifa Stars inahitaji kiungo mchezaji mtoa pasi za mwisho, mtengeneza nafasi na kuitwa kwa Sure Boy ndiyo jibu haswa.
    Kuhusu Kichuya, tangu mechi na Uganda mjini Kampala Novemba 8 na hadi kwenye mchezo wa kwanza na Cape Verde mjini Praia, umuhimu wake ulionekana na utaonekana zaidi Novemba 18 Mungu akimjaalia uzima akaanzishwa. Kila la heri Taifa Stars. Zamu yetu AFCON 2019 Cameroon.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KICHUYA NA SURE BOY WALIKUWA WANAKOSEKANA STARS VITA YA KUWANIA TIKETI YA AFCON 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top