• HABARI MPYA

  Saturday, November 10, 2018

  AZAM FC WASEMA HAWAJATOSHEKA NA KUONGOZA LIGI KUU, WANAONGEZA MAKALI ZAIDI HADI WATWAE UBINGWA MSIMU HUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BENCHI la ufundi la Azam FC limejipanga vilivyo kuwajenga wachezaji kisaikolojia na kisawasawa ili kuendelea na rekodi nzuri waliyoanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu hadi watwae ubingwa.
  Baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, bao pekee la mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, Novemba 4, mwaka huu, Azam FC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 30 kufuatia kushinda mechi tisa na sare tatu huku ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.
  Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, alisema kuwa bado hawajaridhika wao kama benchi la ufundi na wachezaji kwani malengo yao ni kufika pale walipokusudia.  Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi (kulia) amesema hawajaridhika na kuongoza Ligi Kuu, wanataka ubingwa 

  “Tunashukuru mwenendo tunaoendelea kwenda nao na ushindi, ligi bado ndefu hatujaridhika bado hatujaridhika sisi kama makocha tunataka nia yetu tufike pale tulipokusudia na wachezaji vilevile hawajaridhika ina maana kila mechi inayokuja mbele yetu ni fainali tunataka pointi tatu,” alisema.
  Alisema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufakisha kupata pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar huku akiwapongeza wachezaji na viongozi kwa ushirikiano wa pamoja uliofanikisha kupatikana kwa ushindi huo.
  “Licha ya mazingira magumu tuliyopangiwa kucheza saa 8, si muda mzuri kutokana na hali ya hewa iliyopo hapa (Bukoba) ni joto na wakati mwingine tulitegemea mvua lakini leo haikuwepo na kulikuwa na hali ya joto kubwa sana kiasi kwamba wachezaji ni binadamu wanakwenda sehemu vifua vinafunga.
  “Tuliweza kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu sana tunasema kucheza na timu kama Kagera timu ambayo inakaa watu tisa nyuma ya mpira kila wakati ni ngumu sana kuweza kupata magoli mengi lakini niwashukuru wachezaji wameweza kupambana tumeweza kupata goli moja na kulilinda mpaka dakika za mwisho,” alisema.
  Kikosi cha Azam FC kitarejea uwanjani Novemba 22, mwaka huu kumenyana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WASEMA HAWAJATOSHEKA NA KUONGOZA LIGI KUU, WANAONGEZA MAKALI ZAIDI HADI WATWAE UBINGWA MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top