• HABARI MPYA

    Wednesday, November 01, 2017

    YANGA YAWAFUATA SINGIDA UNITED BILA NYOTA WANNE

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Yanga kitaondoka kesho mapema kwa basi lake kwenda Singida kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Singida United Jumamosi Uwanja wa Namfua.
    Lakini wachezaji wanne tegemeo hawakuwemo kwenye msafara na hao ni beki Juma Abdul, kiuno Thabani Kamusoko, washambuliaji Mzimbabwe mwenzake, Donald Ngoma na Mrundi, Amissi Tambwe.
    Abdul hatakuwemo kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, wakati Kamusoko, Ngoma na Tambwe wote ni majeruhi wa muda mrefu.
    Juma Abdul (kulia) hatasafiri na Yanga kwenda Singida baada ya kuonyeshwa kadi ya tatu ya njano wakitoa sare ya 1-1 na Simba Jumamosi
    Yanga inaendelea na mazoezi asubuhi ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kabla ya safari ya kesho kwenda kupambana na timu inayofundishwa na kocha wao wa zamani, Mholanzi, Hans van der Pluijm.
    Yanga inakwenda kwenye mchezo huo, ikitoka kutoa sare na wapinzani wa jadi, Simba kwa kufungana 1-1 Jumamosi iliyopita Uwanja wa Uhuru.
    Sare hiyo imefanya timu hizo ziendelee kufungana kwa pointi 16 kileleni mwa Ligi Kuu, 16 kila moja sawa na Azam FC na Mtibwa Sugar.  
    Ligi Kuu itaendelea Ijumaa, Maji Maji FC wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, wakati Jumamosi Singida watakuwa wenyeji wa Yanga Uwanja wa Namfua, Singida na Ndanda FC wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Mechi nyingine za Jumamosi, Kagera Sugar wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Njombe Mji FC wataikaribisha Mbao FC Uwanja wa Saba Saba na Azam FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Jumapili kutakuwa na mechi mbili, mbali na Mbeya City kuwa wenyeji wa Simba, Lipuli FC nao wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAWAFUATA SINGIDA UNITED BILA NYOTA WANNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top