• HABARI MPYA

    Tuesday, November 21, 2017

    OKWI ASIKITIKA KUKOSEKANA UWANJANI…ASEMA ATARUDI IMARA NA KUISAIDIA SIMBA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Mganda wa Simba SC, Emmanual Okwi amesema kwamba atarejea uwanjani kwa nguvu atakapopona maumivu yake madogo yaliyomuweka nje kwa wiki mbili.
    Okwi aliumia mazoezini katika timu yake ya taifa, Uganda na hakuwpo Uwanja wa Umoja mjini Brazzaville wakati  The Cranes inalazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji Novemba 12, mwaka huu.
    Akakosekana pia Novemba 18 wakati klabu yake, Simba SC inawachapa 1-0 wenyeji, Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bata Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Na baada ya kukosekana kwa muda wote huo uwanjani, Okwi amesema; “Hakika nimeikosa soka. Lakini nitarejea mwenye nguvu mara tu nitapopona maumivu yangu madogo,”.
    Emmanual Okwi amesema atarejea uwanjani kwa nguvu atakapopona maumivu yake 

    Na Okwi anayasema haya wakati ushindani katika ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaongezeka.
    Baada ya mechi 10 za awali, Simba SC wapo kileleni kwa pointi zao 22, sawa na Azam FC wanaokaa nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao, wakati mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 20 ni wa tatu.
    Na kwenye ufungaji wa mabao, Mzambia Obrey Chirwa wa Yanga amemkaribia Okwi kwa mabao baada ya Jumapili kufunga mabao matatu katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Okwi anaongoza kwa mabao yake nane, akifuatiwa na Chirwa mwenye mabao sita sawa na Mohammed Rashid wa Prisons, wakati Ibrahim wa Yanga, Eliud Ambokile wa Mbeya City na Habib Kiyombo wa Mbao FC wana mabao matano kila mmoja. 
    Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea Ijumaa, wenyeji Ndanda FC wakiwakaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Jumamosi, Yanga wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na  Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida.
    Mechi nyingine za jumamosi, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
    Jumapili Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Azam, Complex na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI ASIKITIKA KUKOSEKANA UWANJANI…ASEMA ATARUDI IMARA NA KUISAIDIA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top