• HABARI MPYA

  Monday, November 06, 2017

  NDEMLA KUONDOKA KESHO SIMBA KWENDA SWEDEN TIMU YA ULIMWENGU

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa Simba SC, Said Hamisi Ndemla anatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Sweden kufanya majaribio katika klabu ya AFC Eskilstuna.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema leo katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari kwamba, Ndemla atakuwa Sweden kwa wiki mbili kujaribu bahati yake katika timu hiyo ya Ligi Kuu ya nchini humo, maarufu kama Superettan.
  “Klabu inaamini Ndemla atafanya vizuri na kufuzu katika majaribio hayo, na kama itakuwa tofauti na hivyo, mchezaji huyo ataendelea kuichezea Simba. Huu ni utaratibu wa klabu wa kuwapa nafasi wachezaji wake kwenda nje kujaribu bahati zao za kucheza soka ya kulipwa,” amesema Manara.
  Said Ndemla anatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Sweden kufanya majaribio katika klabu ya AFC Eskilstuna

  Akifanikiwa kufuzu majaribio katika klabu hiyo, Ndemla mwenye umri wa miaka 21 ataungana na Mtanzania mwingine, mshambuliaji Thomas Ulimwengu, ambaye hata hivyo kwa sasa ni majeruhi anasumbuliwa na maumivu ya goti tangu Septemba, mwaka huu na atakuwa nje hadi Januari mwakani.
  Ndemla aliibukia kikosi cha timu ya vijana ya Simba, maarufu kama Simba B mwaka 2012 kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa mwaka 2013 na tangu mwaka 2015 amekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu amehamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDEMLA KUONDOKA KESHO SIMBA KWENDA SWEDEN TIMU YA ULIMWENGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top