• HABARI MPYA

  Tuesday, November 07, 2017

  MBEYA CITY WAWASILISHA MALALAMIKO RASMI TFF ‘BAO LA OFFSIDE’, WATOA NA REKODI YA REFA KIKUMBO KUIBEBA SIMBA

  Na David Nyembe, MBEYA 
  UONGOZI wa timu ya Mbeya City umeandika barua Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulalamikika kutotendewa haki katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
  Mbeya City ilichapwa 1-0 Jumapili na Simba, bao pekee la Shiza Ramadhani Kichuya katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amesema kwamba uchezeshaji wa refa Ahmed Kikumbo aliyesaidiwa na Omar Juma wote wa Dodoma na Michael Mkongwa kutoka Njombe haukuwa wa haki kwa mujibu wa sheria 17 za soka.
  Mbeya City ilichapwa 1-0 Jumapili na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Sokoine 

  Kimbe ambaye amesema bao walilofunga Simba lilikuwa la kuotea dhahiri, amesema wamekwishawasilisha barua TFF wakiainisha maeneo ambayo refa Kikumbo alitoa maamuzi ya utata.
  Kimbe ameitaka Bodi ya Ligi ya TFF kumchunguza refa huyo, kwani amekuwa na rekodi ya kutoa maamuzi ya utata yenye kuisaidia Simba baada ya Mei mwaka huu pia kutoa penalti ya utata katika fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ambayo Simba waliitumia kupata bao la ushindi wakiilaza 2-1 Mbao FC. 
  “Sasa sisi tumewaandikia barua TFF na tumeyaeleza yote hayo, ni jukumu lao kuyafanyia kazi, maana hatuwezi tukakaa kimya huku tukiona kabisa hatutendewi haki,”amesema Kimbe.
  Pamoja na hayo, Kimbe amelalamikia kitendo cha Bodi ya Ligi kuwapa taarifa ya kumfungia kipa wao, Mmalawi Owen Chaima siku moja kabla ya mechi na Simba kwa kosa analodaiwa kufanya wiki moja iliyotangulia.
  Kimbe amesema Chaima anatuhumiwa kumpiga kibao beki wa Azam FC, Yakubu Mohammed katika mchezo wa Oktoba 27, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, lakini taarifa ya kusimamishwa kwake hadi suala lake litakapotolewa maamuzi na Kamati ya Nidhamu iliwasilishwa Ijumaa. 
  “Hii si maana ya Kamati ya Saa 72, mechi imechezwa Oktoba 27 na taarifa tunapewa Novemba 4, nadhani hapa kuna mapungufu, kwa hii tumewaandikia tu TFF, ili wajue na warekebishe utaratibu wao. Malalamiko yetu ya msingi ni uchezeshaji wa refa tu,”amesema.
  Katika hatua nyingine, Kimbe amesema kwamba kikosi kinatarajiwa kuondoka Mbeya kwenda Kilimanjaro na Tanga kwa ajili ya mechi za kirafiki kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga Novemba 19 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  “Tukiwa Kilimanjaro tutacheza na Polisi na tukienda Tanga tutacheza na Coastal Union na African Sports,”amesema Kimbe.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY WAWASILISHA MALALAMIKO RASMI TFF ‘BAO LA OFFSIDE’, WATOA NA REKODI YA REFA KIKUMBO KUIBEBA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top