• HABARI MPYA

    Friday, November 03, 2017

    MAYANGA AWAENGUA KIKOSINI STARS NYONI NA MUZAMIL, AWACHUKUA MUDATHIR NA MKUDE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Shaaban Mayanga amewaengua kwenye kikosi chake wachezaji wawili wa Simba, beki Etasto Nyoni na kiungo Muzamil Yassin kuelekea mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin wiki ijayo.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema wachezaji hao wameenguliwa kutokana na kutolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita dhidi ya Malawi Oktoba 7, mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Lucas amesema katika utaratibu wake mpya, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linaagiza mchezaji anayeonyeshea kadi nyekundu hata katika mchezo usio wa mashindano, asitumike katika mchezo unaofuata.
    Muzamil Yassin (kushoto) ameenguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars

    “Sasa baada ya kupokea barua ya FIFA ikituzuia kuwatumia wachezaji hao katika mchezo ujao dhidi ya Benin, kocha amefanya mabadiliko hayo madogo,”amesema Lucas.
    Lucas amesema kwamba baada ya kuenguliwa kwa Nyoni na Yassin, Mayanga amewaita viungo Mudathir Yahya kutoka Singida United na Jonas Mkude kutoka Simba SC. 
    Baada ya kucheza nyumbani mfululizo mechi za kirafiki za kimataifa, Taifa Stars sasa itatoka mwezi ujao kwenda Benin kucheza na wenyeji Novemba 11, mwaka huu na kikosi cha wachezaji 24 kitaingia kambini Novemba 5 mjini Dar es Salaam kabla ya kusafiri Novemba 9 kwenda Benin tayari kwa mchezo huo.  
    Kikosi kamili cha Taifa Stars sasa ni makipa; Aishi Manula (Simba SC), Peter Manyika (Singida United) na Ramadhani Kabwili, mabeki Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afruka Kusini), Gardiel Michael (Yanga), Kevin Yondan (Yanga), Nurdin Chona (Prisons) na Dickson Job (Mtibwa Sugar).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Mudathir Yahya (Singida United), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Jonas Mkude (Simba), Raphael Daudi (Yanga), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Ibrahim Hajib (Yanga), Mohammed Issa (Mtibwa), Farid Mussa (Tenerife/Hispania) na Abdul Mohammed (Tusker/Kenya) na washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Mbaraka Yussuf (Azam FC), Elias Maguri (Huru) na Yohanna Nkomola (Huru).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANGA AWAENGUA KIKOSINI STARS NYONI NA MUZAMIL, AWACHUKUA MUDATHIR NA MKUDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top