• HABARI MPYA

  Monday, November 06, 2017

  KINDA MKALI WA MABAO AZAM, YAHYA ZAYED AAHIDI MAMBO MAZURI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa Azam FC, Yahya Zayed, amewaambia mashabiki wa timu hiyo washushe presha, kwani mambo mazuri zaidi yanakuja.
  Kauli ya kinda huyo imekuja muda mchache mara baada ya kufunga bao muhimu usiku wa Jumamosi, lililoihakikishia pointi tatu muhimu Azam FC wakati ikiichapa Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Hilo linakuwa ni bao lake la tatu kuifungia Azam FC baada ya kupandishwa akitokea timu ya vijana ya timu hiyo (Azam U-20), na bao lake la kwanza linalomtambulisha kwenye ligi hiyo, mengine mawili akifunga katika mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu mpya la kwanza akitupia dhidi ya Lipuli (4-0) na jingine Azam FC ilipoilaza Onduparaka ya Uganda mabao 3-0.
  Yahya Zayed, amewaambia mashabiki wa Azam washushe presha mambo mazuri zaidi yanakuja 

  Akizungumzia ushindi huo, Zayed alisema kwamba ni jambo la faraja kwake kuweza kuifungia bao muhimu timu hiyo huku akisema bao hilo limemfungulia njia ya kufanya vizuri zaidi kuelekea mechi zinazokuja.
  “Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuisaidia timu yangu kuibuka na pointi tatu, haikuwa kazi rahisi kupata ushindi huo tumepambana kwa dakika zote na hatimaye mwishoni tukafanikiwa kuibuka na ushindi, hii ni historia kwangu.
  “Mashabiki wasikate tamaa waendelee kutuunga mkono na washushe presha kwani mambo mazuri zaidi yanakuja, tunawaomba waje kwa wingi uwanjani kutushangilia hata pale tunapokosea basi waendelee kututia nguvu kwa kutushangilia,” alisema Zayed.
  Ushindi huo uliiwezesha Azam FC kufikisha jumla ya pointi 19, sawa na Simba ambao jana waliifunga Mbeya City bao 1-0 mjini Mbeya katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
  Lakini hadi sasa timu zote za ligi hiyo zikiwa zimeshacheza mechi tisa, Azam FC imeonekana kuwa na safu kali ya ulinzi kwani inashikilia rekodi ya kufungwa mabao machache, ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KINDA MKALI WA MABAO AZAM, YAHYA ZAYED AAHIDI MAMBO MAZURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top