• HABARI MPYA

  Friday, March 17, 2017

  ZANACO WATAKA KUWAPELEKA YANGA UWANJA WA MASHUJAA

  Na Jeff Leah, LUSAKA
  TIMU ya Zanaco inataka kuutumia Uwanja wa Taifa wa Mashujaa mjini Lusaka kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga SC ya Dar es Salaam Jumamosi wiki hii.
  Mabingwa hao wa Zambia wamejiandaa kuutumia Uwanja huo unaochukua mashabiki 60,000 kwa ajili ya michuano ya Afrika.
  Uwanja wa Mashujaa hivi karibuni ulitumika kwa Fainali ya michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 Afrika ambayo wenyeji Zambia walishinda 2-0 Machi 12 dhidi ya Senegal.
  “Bado haijathibitishwa rasmi na bado tunajadiliana nao (uongozi wa Uwanja wa Mashujaa) juu ya kuutumia Uwanja wa Taifa wa Mashujaa,” amesema kocha wa Zanaco, Numba Munamba.
  Zanaco inataka kuutumia Uwanja wa Taifa wa Mashujaa mjini Lusaka kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa na Yanga 

  Tayari Zanaco imekwishacheza mechi mbili Uwanja wa Taifa wa Mashujaa msimu wa mwaka 2016, walipoikaribisha Nkana Julai 2 na wenyeji hao kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kuutumia tena wakifungwa 1-0 na Zesco United katika fainali ya Kombe la Barclays 2016 Novemba 26.
  Zanaco hawautumii Uwanja wao wa Sunset kwa ajili ya mechi za michuano ya Afrika, bali Uwanja wa Nkoloma.
  Kikosi cha Numba kitawakaribisha Yanga Machi 18 katika mchezo wa marudiano baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 11 na wanahitaji ushindi ili kwenda hatua ya makundi, wakati timu itakayofungwa itaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZANACO WATAKA KUWAPELEKA YANGA UWANJA WA MASHUJAA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top